Saturday 9 November 2013

Selemani Uliza:‘Ninaishi kwa kuosha maiti kwa miaka 30’

Dar es Salaam. Naingia katika lango kuu la chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Watu wengi wamesimama katika makundi, baadhi yao wakiwa na sura zilizojaa simanzi.
Hawa wanasubiri kuchukua au kuaga miili ya marehemu waliolala katika chumba hiki. Mlango wa kwanza wa chumba hiki ni mapokezi, hapa kuna vurugu za hapa na pale  kwa kuwa ndipo watu wanapopata stakabadhi za kutunzia miili ya ndugu zao.
Wengine wamekuja kuwatafuta jamaa zao waliopotea na baadhi wamekuja kuchukua miili iliyopo.
Mlango wa pili yapo majeneza matatu  ambayo tayari yana miili ya marehemu ndani, hawa wameshasafishwa, kupambwa tayari kwa kusafirishwa, kuagwa kisha kwenda kuzikwa.
 Kushoto kuna njia ndogo  inayoelekea yalipo majokofu ya rangi ya fedha. Simanzi imetawala katika eneo hilo lenye harufu ya mauti, kwani humu ndimo ilimolala miili ya marehemu, ambao wanaweza kuwa ni ndugu, jamaa na marafiki zetu. 
Katika njia hii kushoto, kuna chumba, humu wapo wanaume watatu wanamsafisha maiti mwenye jinsi ya kiume.
Amelala katika sinki, mpira wa maji ukimimina maji juu yake, huku mikono ya mmoja wa wanaume, ikimsafisha kwa ustadi mkubwa.
 Katika moja ya dirisha, kuna kitu mfano wa kabati ambacho kimejaa vipodozi vya kila aina, kuanzia wanja, rangi ya mdomo, mafuta, manukato, mkasi, viwembe na sabuni.
Mmoja kati ya watu wanaofanya kazi hii adimu ya kusafisha miili ya marehemu ni Selemani Uliza  anayesema, amesafisha miili ya marehemu kwa miaka 30 sasa.
Anasema kwa kawaida maiti inapofika huhifadhiwa katika jokofu hadi pale ndugu watakapofika na kutaka huduma nyingine zaidi ya kuhifadhi.
“Ndugu huja kumtambua marehemu wao,  wakitaka kusafishiwa, basi sisi hufanya kazi hiyo kwa moyo mweupe tena na kwa ari kuu ya kazi,” anaeleza.
Anasema kiutaratibu,  Hospitali ya Taifa ya Muhimbili hawalazimishi ndugu kuwatumia wahudumu wa chumba cha maiti kusafisha miili hiyo, bali iwapo ndugu watahitaji kupata huduma hiyo, basi watalipia na marehemu 
Gogo Mzome, Mkuu wa kitengo hiki cha kuhifadhi miili anasema bei iliyowekwa na Hospitali ya Muhimbili kusafisha miili ya marehemu ni Sh40,000 kwa maiti moja.
Wanavyofanya kazi
Uliza anasema  wakati wa kusafisha miili hiyo kwanza maiti hutolewa katika jokofu, baada ya hapo huwekwa katika sinki maalumu ambalo linabomba na mpira mwembamba wa kupitisha maji.
Maiti ikishawekwa vyema katika sinki, bomba la maji hufunguliwa na kwa kutumia mpira, maiti huanza kuogeshwa na kusuguliwa kwa sabuni na brashi laini.
“Tunamsafisha kama binadamu yeyote yule anavyotakiwa kusafishwa, tunamsugua na kuhakikisha amekuwa safi. Wakati mwingine tunatumia brashi zenye uwezo wa kutoa uchafu vyema,” anasema.
Baada ya hapo,  anasema maiti hufutwa vyema kwa shuka kisha  taratibu nyingine huendelea iwapo ndugu watahitaji msaada wa aina yeyote kuhusu ndugu yao.
Kwa mfano, iwapo ndugu hawawezi kumvalisha marehemu, Uliza na wenzake humvalisha nguo ambazo zimeletwa kwa ajili ya safari yake hiyo ya mwisho.
Vilevile, iwapo  ndugu watahitaji marehemu wao apambwe, basi Uliza huifanya kazi hiyo ambapo kwa kipindi hicho, chumba hiki hugeuka kuwa saluni ya muda.
“Tunampamba marehemu kwa kutumia kila kifaa ambacho ndugu watahitaji, kwa mfano poda, kama ni mwanamke lipstiki, wanja na manukato. Kama ni mwanaume basi tunamvalisha na kumpaka mafuta,” anasema.
 Anaongeza kuwa: “Kama ndugu watahitaji marehemu avalishwe kito cha dhahabu, huwaita waje kuthibitisha kuwa ndugu yao amevalishwa kito hicho. Unajua siku hizi binadamu hatuaminiki.”
 Baadhi ya ndugu huamua kuleta vito vya thamani vya ndugu zao kama saa, pete, au mavazi yao waliyovaa katika harusi  ili kuwaenzi au kuwaonyesha upendo wa mwisho.
Uliza anasema mbali ya wanawake na wanaume pia husafisha miili ya watoto wachanga. “Naona kawaida tu ninaposafisha miili hii kwa sababu najua huyu ni ndugu yangu, na ninapomsafisha, simchukulii kuwa ni mwanamke, bali marehemu tu wa kawaida,” anasema
Anasema kwa kawaida maiti inapotayarishwa huanza kuvalishwa nguo iwapo ndugu watataka na kisha sanda hufuatia mwishoni, kabla ya kuingizwa kwenye jeneza.
Iwapo maiti inasafirishwa basi huchomwa dawa aina ya ‘Formalin’ maalum kwa ajili ya kuhifadhi mwili wa marehemu usiharibike.
Sindano hiyo huchomwa katika mshipa mkubwa wa damu  na mara nyingi paja hupasuliwa ili kuupata mshipa huo na kiasi cha lita tano ya formalin huwekwa katika mwili huo.
“Lita tano za formalin huifanya maiti isiharibike kwa zaidi ya miezi miwili,” anasema.
Miongo mitatu ya kazi
Uliza alianza kazi hii Januari 1983, na tangu wakati huo anasema hajawahi  kuacha kufanya kazi licha ya kupata mapumziko ya wiki moja au mbili tu.
Anasema alipoanza kazi hii alikuwa na umri wa miaka 28 na alikuwa hajaoa, lakini hata baada ya kuoa na sasa ana watoto wanane, ameendelea kuifanya kazi hii kwa moyo.
“Si umaskini tu unaomfanya mtu afanye kazi fulani, lakini kama ni moyo na uzalendo. Ningeweza hata kufanya kazi ya kuuza samaki au kupika pombe, lakini nilishawishika kuifanya hii” anasema.
 Tangu mwaka  1983, Uliza amekuwa akisafisha si chini ya miili mitatu hadi minne kwa siku, jamboambalo huenda likamfanya kuwa mmoja wa watu wanaosafisha miili mingi zaidi hapa nchini.
 Anasema tangu alipoanza kazi hii amekuwa akiingia zamu tatu, yaani anaingia asubuhi hadi saa 9:00 alasiri na anatoka ili kupumzika na kurudi tena saa 2:00 usiku hadi saa 9:00 alasiri ya siku inayofuata.
Hata hivyo, anasema kazi yake huwa nyepesi kidogo usiku kwa sababu hakuna  watu wengi wanaokuja kuchukua miili ya ndugu zao, ukilinganisha na mchana.
“Mara nyingi usiku, maiti chache hufika hasa zile za wodini au polisi wanaweza kuleta mwizi aliyepigwa, jambazi au mtu aliyepata ajali” anasema.
 Siku asiyoweza kusahau
Mzee Uliza anasema licha ya kuifanya kazi hii kwa miaka 30 sasa na kukutana na mambo mengi , lakini siku asiyoweza kusahau ni hivi karibuni ambapo maiti ya kijana aliyegongwa na treni huko Pugu ilipoletwa chumba cha maiti.
“Nimeifanya kazi hii kwa miaka mingi na nina ujasiri mkubwa tu wa kusafisha miili ya marehemu, lakini juzi niliingiwa na simanzi  na picha niliyoiona ilikuwa ya kutisha” anasema.
 Anasema maiti hiyo ya kijana John Urassa aliyegongwa na treni maeneo ya Pugu, ilikuwa imecharangwa vipande vipande  kiasi cha kushindwa kutazamika.
Kutokana na hali  ya maiti hiyo ilimbidi  Uliza na wenzake waanze kuishona maiti hiyo kwa kuunganisha kipande hadi kipande hadi ikarudi katika umbo kamili kisha wakaanza kuifanyia huduma nyingine.
“Kuna sindano maalumu na tunatumia uzi wa kushonea viatu ambao tulitumia katika kuunganisha  kila kiungo kwa yule kijana. Baada ya hapo tulimsafisha kuondoa damu, kisha akavalishwa sanda na kuwekwa katika jeneza,” anasema.
Changamoto za kazi
Uliza anasema  yeye pamoja na wenzake hukumbana na wakati mgumu pale inapoletwa maiti ya mama mjamzito na kisha ndugu zake kuomba mtoto aliye tumboni atenganishwe na mama yake.
“Inabidi tumchane tumboni, tumtoe mtoto kisha kumshona mama yule kwa uzi na sindano. Ni kazi ambayo inatisha kidogo…yahitaji moyo,” anasema.
Hata hivyo, Uliza anasema, iwapo ndugu watakubali azikwe hivyohivyo basi marehemu huoshwa akiwa na mimba hiyo na kuzikwa kama kawaida.
Changamoto nyingine wanayokutana nayo Uliza anasema ni baadhi ya watu ambao hupenda kulalamika  na kuwakosoa bila ya kujua taratibu za kazi zao.
“Kwa mfano, kwa kawaida mwili wa marehemu hufanyiwa uchunguzi na daktari kila siku saa 4:00 asubuhi, lakini mtu hufika hapa saa 6:00 mchana na kulazimisha marehemu wake afanyiwe uchunguzi wakati anaotaka yeye,” anasema.
Uliza anasema tatizo lingine la maiti kukosa ndugu hasa zile zinaletwa na askari Polisi na kwamba zikikaa sana huwaita manispaa kuzichukua kwa ajili ya kuzika.
Mzome anasema kisheria maiti hutakiwa kuhifadhiwa kwa siku 14 tu kama ni mkazi wa Dar es Salaam na siku 30 kwa wanaotoka mikoani, hivyo muda huo ukipita basi manispaa huzichukua na kwenda kuzika.
chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment