Saturday 9 November 2013

Wamiliki wa blog waipinga TRA

WAMILIMI wa magazeti tando ‘blog’ wamepinga agizo la Mamlaka ya  Mapato nchini (TRA) kulipakodi.
Wakizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, baadhi ya wamiliki hao walisema uamuzi huo si sahihi,  kwani walitakiwa kupanga makundi ya nani anatakiwa kulipa na nani hastahili kulipa, kwani blog zingine ziko kwa ajili ya kutoa taarifa na si vinginevyo.
Kutokana na hali hiyo waliitaka mamlaka hiyo kutumia hekima na busara kwa kuwaita na kujadiliana nao na kufikia muafaka kuliko kutoa agizo bila kwashirikisha.
TRA ilitoa agizo hilo juzi katika mwendelezo wa Wiki ya Mlipakodi.
Mmiliki wa blog ya Bongo Weekend, Khadija Kalili, alisema agizo hilo la  TRA ni kurudisha nyuma harakati za wanahabari katika njia mbalimbali za  kurahisisha upatikanaji habari na pia ni njia ya kuwabana.
Alisema uamuzi huo umemsikitisha kwa kuwa TRA wanafikiri wamiliki wa blog nchini wanapata fedha nyingi, jambo ambalo ni tofauti kwani wanachopata ni kidogo na hakilipwi kwa wakati.
“Ni kweli tunapata matangazo, lakini mengine tunapewa na kuyatoa kirafiki tu kwa ajili ya kupendezesha blog zetu, lakini pia TRA inapaswa kufahamu hatulipwi kwa wakati,” alisema Kalili.
Naye Dina Zubeiry anayemiliki blog ya Dinaismail.blogspot.com, alisema TRA ilipaswa kuwaita kuzungumza na wamiliki wote ili kuchuja, lakini agizo lililotolewa halikuwatendea haki.
Wamiliki wa blog za Habari Mseto  na Tanzania liveblogspot.com, Francis Dande na Yusuf Badi, walisema kufanya hivyo ni sawa na kuwaonea, kwani hata Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)  walishaliona hilo kwamba ndiyo kwanza wanaanza na hakuna kikubwa kinachopatikana.
Hata hivyo, mmiliki wa blog ya Mtaa kwa Mtaa, Othman Michuzi,  alisema suala hilo linawezekana  kwani  ni sehemu ya biashara.
Michuzi alisema kwa upande wake hakuwa na taarifa na hilo, lakini halimpi shida.
“Tuna blog tatu ambazo zimesajiliwa na ziko chini ya Michuzi Media, sisi tunalipa kodi kama kampuni, hivyo ni sawa kwa wamiliki kulipa kodi kwa kuwa tunafanya biashara, hususani katika matangazo,” alisisitiza  Michuzi.
chanzo:tanzania daima

No comments:

Post a Comment