Saturday 16 November 2013

Nabii Elisha Mliri, mume wa marehemu Angela Chibalonza adaiwa kubaka, polisi wamlinda

MCHUNGAJI wa Kanisa la Shakinah Pentecostal la mjini Dodoma, Nabii Elisha Mliri, ambaye pia ni mume wa marehemu Angela Chibalonza, aliyekuwa mwimbaji wa nyimbo za Injili, anatuhumiwa kumpa mimba mwanafunzi wa kidato cha tatu wa Shule ya City High School(jina linahifadhiwa).
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Mary Mkombola (49) alidai kuwa mwanaye alikuwa akisumbuliwa na mapepo, hivyo akaamua kumpeleka kwa Nabii  Elisha  ili aweze kuombewa tatizo hilo lililokuwa likimsumbua.
Mama huyo alisema kuwa mara baada ya kumpeleka binti yake, alifanyiwa maombi na nabii huyo na kisha kuelezwa kuwa alikuwa anasumbuliwa na pepo ambalo pia lingemharibia masomo yake.
Kwa mujibu wa mama huyo, baada ya mchungaji kumfanyia maombi  binti yake, alimwambia kuwa atamsaidia kumsomesha kwa kumlipia ada ya mwaka mzima kutokana na yeye kuwa mjane.
“Alimdanganya atamlipia ada ya mwaka mmoja sh 400,000 ili aendelee na masomo halafu akaniambia kuwa ataniombea na mimi ili niweze kupata uwezo wa kuendelea kumsomesha,” alisema mama huyo.
Aliongeza kuwa mara baada ya kukubaliana na mtoto wake, alipeleka taarifa shuleni ambako aliambiwa apeleke barua ya kuthibitisha kuwa atakuwa anamlipia ada mwanafunzi huyo.
Mkombola alifafanua kuwa aliongeza kuwa mara baada ya kupeleka barua shuleni na kukubaliwa, mtoto huyo aliendelea na masomo yake lakini baadaye alianza kumhisi ni mjamzito.
Alisema kuwa alimuuliza kama ana ujauzito akawa hataki kumwambia ndipo akaamua kumchapa na kukimbilia kwa mama yake mkubwa maeneo ya Mbwanga.
“Alipokimbilia kule ndipo akaenda kuwaeleza mama zake wakubwa kuwa mama ananipiga wakati mimba nimeipata kule alikonipeleka nikafanyiwe maombi, ikabidi wanipigie simu na kuniambia kuwa mwanangu ana ujauzito na amepewa na Nabii Elisha.
“Nilimuuliza akanisimulia mambo yote ambayo amekuwa akifanyiwa na nabii huyo tangu alipopelekwa kufanyiwa maombi mwezi Machi mwaka huu,” alisema.
Mama huyo aliongeza kuwa waliamua kwenda polisi kutoa taarifa na kupatiwa fomu ya matibabu kwa ajili ya vipimo ambapo binti  huyo aligundulika kuwa ana ujauzito.
Alisema kuwa walipeleka majibu hayo polisi na kutoa maelezo ambapo waliambiwa kuwa wasubiri uchunguzi unaendelea na utachukua muda mrefu.
“Tulitoa maelezo polisi mimi na mwanangu na kuambiwa kuwa tusubiri bado wanafanya uchunguzi lakini muda umepita sasa na mtoto tumbo linazidi kukua na masomo kasimama bila kujua hatima yake,” alisema.
Alibainisha kuwa mara baada ya baadhi ya viongozi wa kanisa hilo kupata taarifa, walimfuata mama huyo wakimsihi asilipeleke suala hilo polisi bali wao watalimaliza.
“Walinifuata watumishi wawili ambao ni Nabii Mgamba na Nabii Monika wakasema nisifanye lolote wao watamtunza au kama ikiwezekana tuitoe mimba hii, jambo ambalo sikukubaliana nalo,” alisema.
Naye mwanafunzi huyo alisema kuwa Juni 8, mwaka huu, asubuhi alipigiwa simu na Nabii Elisha akamwambia aende mjini na alipofika alimpakia kwenye gari lake na kwenda naye kwenye nyumba ya kulala wageni iliyoko maeneo ya jirani na Chuo cha CBE mjini hapa.
“Nilimuuliza tunakwenda wapi, akaniambia tunakwenda kanisani lakini cha kushangaza tulilipita kanisa, hivyo nikawa na wasiwasi lakini kabla hatujafika tulikokuwa tunakwenda tukapita sehemu akaongeza upepo kwenye tairi,” alisema.
Kwamba baada ya kujaza upepo, waliondoka na kwenda katika nyumba hiyo ya kulala wageni lakini kabla hawajashuka alimpatia soda aina ya Fanta akanywa na muda mfupi akapoteza fahamu kidogo na alipozinduka akajikuta anafanya mapenzi na mchungaji huyo.
“Nilijikuta kifuani mwa nabii tukiwa wote watupu, nikaanza kulia, akanibembeleza na kuniambia ‘unafikiri kukulipia ada yote hiyo ilikuwa ni bure’ mbona wapo watu wengi sijawalipia ada, lazima nifanye na wewe mapenzi mara tano, kwa hiyo bado mara nne nitafanya na wewe hata kwa nguvu na ukimwambia mtu nitakuua kwa maombi,” alisema.
Binti huyo alidai kuwa tangu siku hiyo hakuweza kuziona siku zake tena mpaka mama yake alipoanza kumhisi kuwa ana ujauzito na kumpeleka kupima na kubainika ni kweli.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Suzan Kaganda, alithibitisha kuwa tayari walikwisha kuyapokea malalamiko ya mwanafunzi huyo na wanayafanyia kazi.
“Tunayafanyia kazi, kwani tulipata malalamiko hayo lakini tunasubiri hadi atakapo jifungua tuweze kutumia kipimo cha vinasaba (DNA) kuthibitisha aliyempa ujauzito,” alisema.
Alipotafutwa Nabii Elisha alisema kuwa hayuko Dodoma kwa wakati huu na kumtaka mwandishi aende polisi atapata maelezo zaidi.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment