Saturday 16 November 2013

Papa Msoffe awekwa ‘kiporo’

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya mauaji inayomkabili mfanyabashara maarufu jijini Dar es Salaam,  Abubakar Marijan (50) maarufu kama Papaa Msoffe na  Makongoro Joseph Nyerere umedai kuwa jalada la kesi hiyo tayari limeshatoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka  (DPP) na sasa liko kwa  Mkurugenzi wa  wa Makosa ya Jinai (DCI).
Mwendesha Mashtaka Inspekta wa Polisi, Hamisi Said, jana aliikumbusha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa kesi hiyo ilikuwa kwa ajili ya kutajwa na kuangalia maendeleo yake.
Alieleza kuwa jalada la kesi hiyo ambalo lilienda kwa DPP, aligundua lina mapungufu akamwelekeza DCI alifanyie marekebisho na kwamba tayari DCI amefanyia kazi, hivyo muda wowote litarejeshwa mahakamani hapo kwa ajili ya hatua zaidi.
Hakimu Hellen Liwa aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 27, mwaka huu, itapokuja kwa ajili ya kutajwa na kuamuru washtakiwa wapelekwe mahabusu.
Katika hatua nyingine, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Aloyce Katemana, alitupilia mbali ombi la vigogo wa SUMA JKT wanaokabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya madaraka.
Ombi hilo lilitaka mahakama hiyo ikatae kupokea maelezo ya onyo yaliyochukuliwa wakati wakihojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kabla hawajafunguliwa kesi mahakamani hapo.
Katemana alisema kuwa TAKUKURU hawakuvunja sheria wakati wakichukua maelezo ya onyo na hivyo aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 12 mwaka huu, ambapo mashahidi wa upande wa jamhuri wataendelea kutoa ushahidi wao
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment