Saturday, 2 November 2013

Zaidi ya mara ya tatu sasa kesi ya PAPA MSOFE yawa MAUZAUZA.


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kwa zaidi ya mara ya tatu sasa imejikuta ikishindwa kutoa uamuzi wake wa ama kumfutia kesi ya mauaji au la inayomkabili mfanyabiashara maarufu jijini hapa, Abubakar Marijan (50), maarufu kama ‘Papaa Msoffe’ na Makongoro Joseph Nyerere, kwa madai kuwa jalada la kesi hiyo limepelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Wakili wa Serikali, Charles Anindo, aliikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwa ajili ya mahakama kutoa uamuzi wake wa ama kuwafutia kesi washitakiwa au la, ila upande wa Jamhuri umepeleka jalada la kesi hiyo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu kesi hiyo, hivyo akaomba kesi hiyo iahirishwe.
Ombi hilo lilisababisha Hakimu Mkazi, Hellen Liwa, kusema mahakama yake ilikuwa ipo tayari kwa ajili ya kutoa uamuzi wake lakini kwa kuwa upande wa Jamhuri umewasilisha ombi hilo ambalo limeonesha ni dalili nzuri za maendeleo ya kesi hiyo, hivyo anaiahirisha kesi hiyo hadi Novemba 14, mwaka huu.
Siku hiyo itakuja kwa ajili ya kutajwa, kwani inawezekana yakapatikana maendeleo mazuri ya kesi hiyo kutoka upande wa Jamhuri.
Septemba 12, mwaka huu, Wakili Kweka aliwasilisha pingamizi lililokuwa linaomba mahakama hiyo ilikatae ombi la wakili wa washitakiwa, Daudi Malima, lililokuwa likiomba mahakama hiyo iwafutie kesi hiyo kwani ni ya muda mrefu na hadi sasa upelelezi bado haujakamilika.
Februari 13, mwaka huu, Wakili wa Serikali, Charles Anindo, aliiomba mahakama kumuunganisha Nyerere katika kesi hiyo ambayo awali ilikuwa ikimkabili Msoffe peke yake, ambaye alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Agosti 10, mwaka 2012 na kusomewa shitaka.
Washitakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kumuua kwa makusudi Onesphory Kituli, kinyume cha kifungu cha 196 cha Kanuni za Adhabu sura ya 19 kama kilivyorekebishwa mwaka 2002 na kwamba kosa hilo walilitenda Oktoba 11, mwaka 2011, nyumbani kwa marehemu Magomeni Mapipa, jijini Dar es Salaam
chanzo:daima


No comments:

Post a Comment