Monday 16 December 2013

Hizi ndizo sababu za kigogo wa ccm Mabina kuuawa kinyama


Mwenyekiti  mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza, Clement Mabina (56), ameuawa kinyama kwa kushambuliwa na wakazi wa Kijiji cha Kisesa baada ya kutuhumiwa kumuua mwenzao kwa kumpiga risasi kufuatia kuzuka mgogoro wa ardhi baina yao.

Mabina aliuawa jana kwa kushambuliwa na wakazi hao kwa mawe, majembe na mundu kama hasira ya kulipiza kisasi baada ya mwenzao kuuawa kwa kupigwa risasi na kigogo huyo wa CCM.

Chanzo cha mauaji hayo yanadaiwa kuwa ni baada ya Mabina kumkuta mwanakijiji huyo akilima kwenye shamba analodai kuwa ni mali yake.

Inadaiwa kuwa baada ya kufika kwenye shamba hilo, Mabina alimkuta mkazi huyo na wenzake wakilima na alipowauliza ndipo yalipoanza malumbano baina yao.

Inadaiwa kuwa baada ya kuzuka malumbano hayo na ugomvi,  wanakijiji walianza kumshambulia Mabina nae ndipo alipotoa bastola yake kwa lengo la kujihami na kumpiga risasi mmoja wao ambaye alikufa papo hapo.

Baada ya mwenzao kuuawa, wanakijiji hao walipiga yowe kuomba msaada kwa wenzao ambao walikusanyika haraka kwenye eneo hilo na kuanza kumshambulia Mabina kwa silaha mbalimbali za jadi hadi lipokata roho.

Inadaiwa kuwa Mabina alikufa  kutokana na kupata majeraha makubwa mwilini mwake na kutokwa na damu nyingi.

Dereva wake, aliwasha gari na kukimbia huku akimwacha bosi wake akishambuliwa kwa kipigo kutoka kwa wakazi hao akijaribu kwenda kutafuta msaada lakini bila mafanikio.  

Hadi taarifa za mauaji hayo zinaripotiwa Kituo cha Polisi,  mwanakijiji huyo aliyeuawa kwa kupigwa risasi ametajwa kuwa ni Temeli Malemi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kusisitiza kuwa wanaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo chake.

Mabina alikuwa Mwenyekiti wa CCM mkoani Mwanza kuanzia mwaka 2012 hadi alipobwagwa na Dk. AnthonyDialo, katika uchaguzi wa ndani ya chama hicho.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment