Monday 16 December 2013

Mama Maria Nyerere,Kikwete wafunika mazishi ya Mandela

Rais Jakaya Kikwete na mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere, jana walifunika kwenye ibada maalumu ya kumuaga aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, iliyofanyika kijijini kwake Qunu, Mashariki mwa Cape.

Tukio hilo lilitokea baada ya Rais Kikwete kupewa fursa ya kuzungumza kwenye ibada hiyo ambayo ilianza mapema asubuhi.

Rais Kikwete alishangiliwa wakati akizungumzia uhusiano wa Tanzania na Afrika Kusini ulioasisiwa na hayati Mwalimu Julius Nyerere na Mandela wakati akiwaelezea maelfu ya watu kati ya 4,500 waliohudhuria, akiwamo mjane huyo wa Nyerere.

Vile vile, walimshangilia baada ya kuwaeleza kuwa mwingine aliyehudhuria ibada hiyo ni Vicky Swai, ambaye Mandela alisahau mabuti yake nyumbani kwake alipozuru Tanzania baada ya kutolewa gerezani alikotumikia kifungo cha miaka 29 jela.

Alisema wakati Mandela akizuru Tanzania, wananchi hawakusita kujitokeza kumpokea barabarani licha ya mvua kubwa zilizokuwa zikinyesha wakati huo kutokana na jinsi walivyompenda kutokana na mchango wake katika harakati za ukombozi nchini humo na Afrika kwa jumla.

RAIS KIKWETE AHUTUBIA
Katika hotuba yake, Rais Kikwete kwa sehemu kubwa alizungumzia uhusiano mkubwa uliopo kati ya nchi hizo mbili tangu enzi za Marais, Julius Nyerere na Mandela na jinsi Tanzania ilivyokisaidia Chama cha African National Congress (ANC). 

Alisema mwaka 1962, katika harakati za kupigania uhuru wa nchi yake, Mandela alikuja nchini kwa siri akipitia mkoani Mbeya na kuwasili Dar es Salaam, ambako alikutana na Nyerere kwa siri kuomba msaada zaidi juu ya harakati za ukombozi nchini humo.

Rais Kikwete alisema akiwa nchini, Mandela aliacha viatu vyake aina ya buti kwenye nyumba ya Mama Swai, alikokuwa amelala kabla ya kwenda Algeria, akitumaini kwamba baada ya kurudi angekuja kuvichukua, lakini alikamatwa na kufungwa nchini mwake kwenye Kisiwa cha Roben, kwa miaka 27 hadi alipokuja kufunguliwa mwaka 1992.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, baada ya Mandela kuwa kiongozi wa Jamhuri ya Afrika Kusini mwaka 1995, yeye pamoja na Mama Swai, walimpelekea viatu vyake, na baada ya kuvipokea alisema alikuwa anavikumbuka.

Huku akipigiwa makofi kutoka kwa umati huo, Rais Kikwete alisema Tanzania ilitoa ushirikiano mkubwa kwa Afrika Kusini ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya kijeshi kwa askari wa nchi hiyo katika maeneo ya Mazimbu mkoani Morogoro.

Mbali na taifa hilo, pia Tanzania ilitoa msaada wa kijeshi kwa vyama vya siasa vya MPLA, ANC, Zapu na Frelimo. Rais Kikwete aliuambia umati huo kuwa, yupo pamoja na mama Maria Nyerere, ambaye mumewe hayati Nyerere, alishirikiana kwa karibu na Mandela katika harakati za ukombozi wa taifa hilo, na hivyo kuwafanya kupiga makofi kwa utambulisho huo.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, Tanzania ilitumia Shirika lake la Utangazaji, kutangaza vipindi ambavyo vililenga kutoa elimu zaidi ya kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini na kuleta uhuru wa taifa hilo na kuongeza kuwa Mandela alikuwa rafiki mkubwa wa taifa la Tanzania.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment