Monday 30 December 2013

Mwaka 2014 huooo....umefanya nini 2013?

 Wakati tunaelekea kukamilisha ngwe ya mwaka huu wa 2013, yapo mambo mengi ambayo baadhi yetu waliyapanga kuyatekeleza ndani ya mwaka huu wa 2013, ambayo ni miradi ya maendeleo binafsi, wanaona umuhimu wa kuyakumbuka na kuyatathmini ili kujua kiwango cha ukamilifu wake kabla ya mkesha wa mwaka mpya. 
 
Nina uhakika asilimia kubwa ya mipango ya mikakati ya  wengi yaliyopangwa kukamilishwa ndani ya mwaka huu unaomalizika kesho kutwa hayajakamilika kwa asilimia zote kutokana na hali halisi ya kiuchumi.
 
Hiyo inaweza kuwa moja ya changamoto za kukabiliana kwa kasi na nguvu zaidi kwa mwaka mpya ujao, aidha mbinu na mikakati ya kujiimarisha zaidi kiuchumi ili kufikia malengo tunayojiwekea zinatakiwa ziende sambamba na fursa za ujasiriamali ambazo zipo mbele yetu.
 
Wananchi wengi sasa wanalia kutokana na hali ngumu ya maisha, wanaelekea kutafuta sababu zilizosababisha ugumu huo, na kwa haraka lawama zinaelekezwa kwa serikali iliyopo, maana huko ndiko waliko viongozi ambao wanao wajibu wa kuratibu namna wananchi watakavyoshiriki katika kujitoa katika umaskini. 
 
Bado sijaona miujiza ya kufanikiwa kujiimarisha kiuchumi zaidi  bila ya kutanguliza jitihada za kufanya kazi kwa mbinu za kisasa za kutumia sayansi na teknolojia. 
 
Wananchi pia wanaelewa kuwa ni kwa kufanya kazi tu ndipo wataondokana na adha ya umaskini uliopo, na pia wanaelewa kuwa maendeleo hayaji kwa kukaa na kulaumu taasisi, au labda kwa kufanya maandamano au kwa shinikizo la aina yoyote ile bila kuhusisha jitihada katika kazi.
 
Yapo maeneo ya msingi ambayo wananchi wanaweza kusimama kidete na kudai vichocheo vya kuwaletea maendeleo, pia kuna misingi inayokubalika kwa wananchi kushinikiza uongozi wa juu kuwafungulia milango ya kujipatia maendeleo, ikiwa ni pamoja na kuhoji kupewa unafuu katika maeneo mbalimbali yanayowakwaza kujiimarisha kijasiriamali.
 
Mwananchi hasubiri kiongozi amhamasishe kufanya kazi, anachoweza kuhamasika ni kwa fursa za wazi zinazoweza kutolewa na kumwezesha awekeze nguvu zake na kuzalisha kwa faida ili ajijengee uwezo zaidi wa maendeleo yake.
 
Kinachoweza kuwa kichekesho kwa wengi ni wakati kiongozi anapowashawishi wananchi wasishiriki kufanya kazi za maendeleo yao, kiongozi anayewaambia wananchi wakae tu bila kazi kwani serikali ipo kwa ajili ya kuwaletea maendeleo.  
 
Ni kweli serikali ipo na moja ya majukumu yake ni kuendeleza wananchi wake katika nyanja mbalimbali na kuhakikisha uchumi wa nchi unaongezeka kwa kutumia wananchi wenyewe kufanya kazi zaidi na kulipa kodistahiki.
 
Kwa upande mwingine, ni aibu kubwa kupoteza maisha kwa sababu ya njaa iliyosababishwa na uzembe tu wa kutojihusisha na kilimo, na wakati mwingine hali iliyosababishwa na kushawishiwa tu, kwamba kilimo siyo muhimu kwani chakula kingepatikana tu kutoka kwa serikalini au kwa mjomba!
 
Wakati mmoja katika vikao vya bunge,  Mbunge wa Viti Maalumu, Mhandishi Stella Manyanya (CCM) alitoa tuhuma kuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa amewahi kuwashawishi baadhi ya wananchi wa mkoa wa Ruvuma kuacha kuchangia maendeleo yao.  
 
Kama aliyoyasema Mheshimiwa Manyanya yana ukweli, basi hilo ni jambo la kusikitisha sana kwa kiongozi wa ngazi ya juu anayetegemewa na wengi kuwa chachu ya kuwahimiza wananchi katika shughuli za maendeleo. Itashangaza pia kama kiongozi huyo alitaka wananchi hao waishi kwa miujiza gani. 
 
Inawezekana kuwa Dk. Slaa alighafirika katika matamshi hayo kutokana na hamasa za kisiasa,  kwani hatua ya kuwahamasisha wananchi wasishiriki katika maendeleo yao, huo siyo uongozi unaotegemewa katika hali ya aina yoyote katika jamii, na hasa katika jamii ya nchi maskini kama Tanzania. 
 
Wananchi wanahitaji kuhamasishwa ili washiriki katika uzalishaji wa miradi yote ya maendeleo kwa faida yao. Na hiyo ndiyo moja ya kazi muhimu za viongozi. 
 
Ni dhahiri kuwa ndani ya siasa kunakuwapo na porojo nyingi, lakini upo ukomo wa porojo wakati wa kuwahamasisha wananchi, na hasa kama ni siasa zinazopingana na zile za chama tawala. 
 
Wakati tunaendekea kutathmini kiwango cha maendeleo yaliyopatikana kwa mwaka huu, ni wakati muafaka wa kujipanga vizuri ili kama yapo makosa yaliyofanyika katika mwaka huu, yarekebishwe ili mwaka ujao wa 2014 uwe wa mafanikio zaidi. 
 
Tathmini hii inaanzia katika ngazi ya mtu binafsi, familia, jamii ya vikundi mbalimbali hadi katika kiwango cha mipango ya Serikali. 
 
Yapo masuala mengi ya msingi ya kujitathmini, ingawa kwa serikali wanaweza kuwa na utaratibu wao kwani mwaka wao mpya ni wa matumizi ya Fedha kuanzia Julai mosi ya kila mwaka.  
 
Kwa wananchi walio wengi, ambao wanafahamu nini maana ya maendeleo, wataweza kupambanua kauli za kisiasa ambazo baadhi ni kwa ajili ya kujitafutia umaarufu na nyingine ambazo ni za uhalisia ambazo haziwadanganyi wananchi na kuwapa njozi za kupata maendeleo kwa njia ya miujiza. 
 
Ni vyema kuwaeleza wananchi ukweli wa mambo hata kama unauma kuliko kuwaongopea na kuwarubuni ili kujipatia tiketi ya kuwa kiongozi kwa njia za mkato zilizogubikwa na uzushi.
 
Majukwaa ya kisiasa yasitumike kujenga hoja zisizotekelezeka, hoja zinazowapotosha wananchi, zisitumike kama hila za kuingia katika safu ya viongozi wa umma, wananchi wanahitaji ukweli mtupu, na kwa kiwango kikubwa wananchi wanafahamu kuwa juhudi zao katika kazi ni ukombozi kwao na ishara ya maendeleo yao. 
 
Kutofanya kazi ni kujitafutia janga, na taifa lisilohusisha wananchi wake katika maendeleo ya nchi ni taifa mufilisi.
chanzo:Nipashe

No comments:

Post a Comment