Sunday 1 December 2013

Zitto apata pigo jingine

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), amepata pigo jipya baada ya wabunge wenzake wa chama hicho kuamua kumuondoa rasmi kwenye nafasi yake ya kuwa Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Habari kutoka ndani ya CHADEMA, zinasema kuwa uamuzi wa kumuengua Zitto kwenye nafasi hiyo, ulifikiwa kabla ya mbunge huyo kuvuliwa nyadhifa nyingine za kichama baada ya Kamati Kuu (CC) ya chama hicho kumtia hatiani kwa makosa ya usaliti.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, tayari wabunge wa CHADEMA wameshapitisha azimio la kumvua nafasi hiyo na chama kinaandaa taarifa rasmi kwa mbunge huyo na ofisi ya spika kumhafamisha jambo hilo.
Duru za siasa kutoka ndani ya CHADEMA zilisema kuwa hata kama Zitto asingevuliwa nyadhifa zake kichama, tayari walishapanga kumvua nafasi ya naibu kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni kwa madai ya kutokuwa na imani naye.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Mwanasheria Mkuu na Mnadhimu Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu, alisema kuwa Kamati Kuu ya chama hicho ilitoa maelekezo kwa Kamati ya Wabunge kukaa mara moja na kumvua nafasi yake ya Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzania Bungeni.
“Azimo la CC lilielekeza Kamati ya Wabunge wa CHADEMA kukaa mapema iwezekanavyo kumvua nafasi hiyo isipokuwa nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ambayo amechaguliwa na wabunge wa vyama vyote,” alisema Lissu.
Hivi karibuni, mbunge huyo maarufu nchini, amevuliwa nyadhifa zake zote za uongozi ndani ya CHADEMA na kubaki kuwa mwanachama wa kawaida.
Nafasi alizovuliwa ni Naibu Katibu Mkuu (Bara), Ujumbe wa Kamati Kuu (CC) na Mjumbe wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu.
Mbali ya Zitto viongozi wengine waliovuliwa nyadhifa zao na kubaki kuwa wanachama wa kawaida, ni Dk. Kitila Mkumbo aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu (CC) na Samson Mwigamba aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, ambaye kompyuta yake mpakato (laptop), ilinaswa kutumika kutuma makala inayodaiwa kukichafua chama kwenye mtandao wa kijamii wa Jamii Forum.
Uamuzi huo mgumu na mzito ulifikiwa wakati wa kikao cha Kamati Kuu (CC), kilichofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Blue Pearl jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Inadaiwa kuwa pamoja na mambo mengine, Zitto alikuwa kinara wa mkakati wa kuleta mabadiliko haramu ndani ya chama hicho, huku waasisi wake wakijipa majina ya MM, M1 na M2.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment