Mzozo unaofukuta ndani ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) unatokana na tofauti baina ya baadhi ya wanachama na si jambo linalohusu sera au itikadi ya chama hicho.
Mwanachama wa siku nyingi wa chama hicho, Profesa Mwesigwa Baregu, amesea tofauti iliyopo baina ya wanachama wa Chadema inaonyesha sura ya kutofautiana mtu na mtu kwenye mbinu zinazoweza kutumiwa dhidi ya wengine.
Profesa Baregu aliyasema hayo juzi wakati wa mjadala uliotangazwa na Sauti ya Amerika (VOA) kuhusu mzozo ndani ya chama hicho.
Alisema vyama vya siasa mara nyingi wanachama wanaunganishwa na itikadi pamoja na sera ambazo zinatakiwa kufuatwa kwa kukubaliana kwa pamoja.
Hata hivyo, alisema utofauti uliopo kwenye chama chake sio wa kiitikadi wala za sera badala yake ni tofauti baina ya watu.
“Labda mbinu mwanachama anazotumia kufanya mambo yake tofauti na mwingine sioni kama tofauti zao ni za kiitikadi au kisera.
Inaweza kuwa za kimbinu zikakuzwa na kuonekani ni tofauti za msingi,” alisema.
Alimtaja aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu (Chadema), Dk. Kitilia Mkumbo ni mmoja wao aliyesimamia ilani ya chama hadi ikapatikana na alikuwa ni mwenyekiti wa kusimamia jambo hilo.
Alisema ilani hiyo iliwasaidia katika uchaguzi na kuwawezesha kupata kura nyingi pamoja na kuongeza idadi ya wabunge.
“Mkumbo alikuwa akisimamia ilani ya chama hadi ikapatikana tofauti za mbinu na staili ya mtu na mtu anavyofanya mambo yake tofauti na wengine ndio zimekuja mbele zaidi badala ya msingi kwani sijaona tofauti za kiitikadi,” alisema Profesa.
Aidha alisema alivyofanya utafiti kuhusu vyama vya siasa na historia ya vyama vya siasa kwa ujumla amebaini kuwa vyama vya siasa kwa ujumla sio vizoefu na masuala ya demokrasia.
“Kila mmoja anasema katiba imefuatwa , Katiba kufuatwa ni sawa lakini sasa siasa za kuishawishi, changamoto kubwa ya siasa ni ushawishi na siasa ni kinyume cha kutumia nguvu ni nguvu ya hoja ,” alisema.
Alisema katiba isije ikatumika badala ya ushawishi ambao ndio unajenga umoja na maelewano ndani ya chama na inakipa nguvu chama kukubaliana kwa pamoja.
chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment