MSANII maarufu wa filamu nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’, amekana shitaka linalomkabili la kumuua bila kukusudia msanii mwenzake, Steven Kanumba, aliyefariki dunia alfajiri ya Aprili 7, mwaka 2012.
Licha ya kukana shitaka hilo, Lulu pia alikiri kuwa alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na marehemu Kanumba.
Akisoma maelezo ya awali jana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, mbele ya Jaji Rose Teemba, Wakili wa Serikali Mwandamizi Monica Mbogo, alidai kuwa Lulu alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na alikuwa akimtembelea Kanumba nyumbani kwake.
Alidai kuwa, siku ya tukio Kanumba alikuwa nyumbani kwake na mdogo wake, Seth Bosco na majira ya saa 6 usiku, Kanumba alimwambia mdogo wake wajiandae kwenda kustarehe.
Kwamba, wakati wakijitayarisha, Lulu alifika na kwenda chumbani kwa Kanumba.
Monica aliendelea kusoma maelezo hayo kuwa, baada ya dakika chache, Seth alisikia kelele zilizodai kwanini Lulu alikuwa akisikiliza simu ya bwana yake mbele yake, alieleza kuwa watu wawili walikuwa wakigombana na mshitakiwa akilia.
Pia aliieleza mahakama kuwa, Seth alimuona Lulu akijitahidi kutoka nje na alivutwa kwa ndani na mlango kufungwa.
Ilidaiwa kuwa Lulu alitoka ndani na akamwambia Seth kuwa Kanumba ameanguka chini, ndipo alipokwenda na kumkuta Kanumba amelala sakafuni hajitambui.
Ilielezwa kuwa alimuita daktari wa marehemu aitwae Paplas Kageiya wa Kigogo, kuhusiana na hali ya marehemu na kugundua kuwa alikuwa ameshafariki dunia lakini hakutoa taarifa, zaidi ya kumshauri waende Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Ilidaiwa kuwa Polisi walifika na kuchora ramani na majira ya saa 11 alfajiri Lulu alikamatwa na kuhojiwa, lakini akikana kumuua Kanumba.
Aidha, baada ya uchunguzi ilidaiwa kuwa chanzo cha kifo ni Kanumba kushindwa kupumua kutokana na msukumo ulioko kwenye ubongo, ubongo kupata mtikisiko na alikuwa na uvimbe kwenye ubongo, lakini hakuwa na majeraha nje.
Katika maelezo hayo, Lulu alikiri jina na anwani, kuwa na uhusiano wa kimapenzi na marehemu, siku ya tukio Lulu alimtembelea Kanumba nyumbani kwake, kulikuwa na ugomvi baina yake na marehemu Kanumba.
Kwamba, Lulu alijaribu kutoka nje ya chumba lakini Kanumba akamrudisha ndani na kufunga mlango, baadaye Lulu alifungua mlango na kumwita Seth Bosco ili amueleze kwamba marehemu alikuwa ameanguka chini na kukiri kuwa alikamatwa Bamaga saa 11 alfajiri.
Katika maelezo hayo, Lulu alikiri kuwa hana ubishi kuwa anashtakiwa kwa kosa hilo.
Baada ya maelezo hayo, upande wa Jamhuri ulidai kuwa una mashahidi wanne ambao ni Seth Bosco, Dk. Palpas Kageiya, Ester Zephania na E 6056 Sajenti Ernatus
chanzo:tz daima
No comments:
Post a Comment