Monday 24 March 2014

Kuonyesha penzi lako lote mapema kwa yule umpendaye ni kosa kubwa!!!!

 naamini ujumbe huu utakukuta  u mzima Sijui pa kuanzia ila siku nyingi nimetamani kukuandikia angalau nitoe yaliyo moyoni mwangu.
 
Mimi ni mama wa vijana 2 handsome (watoto wa kiume wawili wazuri), niliolewa miaka 20 iliyopita ila katika ndoa yangu sikuwahi kuwa na amani wala kujua mapenzi ni nini.
 
Ninachotaka kuuliza; hivi mapenzi ni nini, na ili upendwe kuna vigezo gani, kwa nini yule unayempenda anakuona huna maana? Nifanyeje  mimi sijawahi kuona mtu anayenipenda katika miaka yote hii.
 
Sijawahi kusikia mwanaume anayeniambia ananipenda hata kunipa zawadi ya khanga, je, nina shida gani? Najitahidi kuutoa moyo wangu kwa yule nimpendaye lakini anti sijui. Hivi wale wanaopewa magari ,nyumba, vitu kadha na wapenzi wao inakuwaje?
 
Je, hivi kuna mapenzi  kweli dunia hii? Anti yangu, nisikuchoshe ukitaka hadithi nitafute. Nilichotaka kwa leo kuuliza ni hicho, je, kuna mapenzi ya dhati dunia hii au akishapata akitakacho ni basi?! Asante. nitambue kwa jina la MENG FEI). Hivi ndivyo anavyomaliza ujumbe wake.
 
MAJIBU KUTOKA KWA WADAU
…Dada yangu MENG FEI, kwanza kabisa kabla ya yote nakupa pole kwa yale yote yaliyokukuta kwa kipindi cha miaka 20. Pili, napenda nikushauri kuhusu tatizo linalokusumbua katika mapenzi.
 
Kwanza, kuonyesha penzi lako lote mapema kwa yule umpendaye ni kosa kubwa katika mahusiano ya kimapenzi. Kilichotakiwa ni kumfanyia utafiti anayekupenda ili kumjua undani wake na hiyo itakuwa njia ya kwanza, ikifuatiwa na kumpa penzi mwanaume hatua kwa hatua baada ya kupata jibu kuwa ni mkweli.
 
Kumbuka uhusiano huu utakuumiza sana kichwa na kufikia wakati ukatulia na ndipo penzi litakapokuwa katika mstari ulionyooka. (Abadallah wa Malinyi, Ulanga Morogoro). 
 
….Namshauri huyo mama hilo ni tatizo la kiroho kabisa. Kama yuko Dar aje Kawe Kanisa la Ufufuo na Uzima atasaidiwa. ( Mchungaji Anne).
 
…Anti Flora naomba nichangie swali alilouliza dada MENG FEI akitaka kujua je, kuna mapenzi ya dhati kweli? Nami namjibu kama ifuatavyo; mapenzi ya dhati yapo, tena ukimpata akupendaye utatamani usiachane naye. 
 
Mtu wa kukupa kitu siyo kwamba anakupenda kwa dhati wakati mwingine ni giliba tu. Mapenzi ni utu siyo kitu. Wapo baadhi wanaopewa magari, majumba lakini hawana raha nazo, wewe omba Mungu akupe mpenzi mwenye upendo wa dhati.
 
Hayo magari, majumba na kadhalika yatapatikana tu bila kikwazo (automatically). Hili jambo la kumshirikisha Mungu katika mambo yetu watu huliona dogo lakini kwa wenye ufahamu ni jambo kubwa sana. Huo ndiyo ushauri/mchango wangu kwa ndugu yetu mwanafamilia mwenzetu kwenye safu yetu hii ya Maisha Ndivyo Yalivyo.
 
...Tatizo kubwa la mwanaume kupunguza mapenzi kwa mke baada ya kuishi pamoja ni ile hali ya mwanamke aliyomkuta nayo mwanzo. Kwa maana alishatumika, kwa hiyo anajua kabisa alikuwapo mwanzangu kabla yake. Hivyo hamthamini tena (Shirima wa Morogoro). 
 
…Habari wapendwa, huyo dada tatizo lake kubwa ana nyota tatu na zote ni mbaya. 1. Nyota ya bundi 2. Nyota ya chura na  3. Nyota ya fisi. Ndiyo chanzo cha matatizo yake(Gaitan Kamaka, Dar)
 
 Ilibidi katika hili nimtumie ujumbe mfupi kupitia simu ya kiganjani msomaji huyu ili afafanue juu ya nyota hizo mbaya zina maana gani na katika kujibu akasema; nyota ya fisi ni kwamba ana tamaa bila kujua mazingira ya kupendwa yanatengenezwa na hayapatikani kama maji ya mvua.
 
Ile nyota ya  bundi ni kwamba bundi ni mikosi kutokana na tamaa zake anajihisi kama ana mkosi na nyota ya chura anaona kila anapopita anapigwa mateke tu. Hivi ndivyo anavyomaliza ufafanuzi wetu mwenzetu Gaitan.
 
Mwingine anasema;…Habari, mapenzi  ni nini?  Ni upendo baina ya mtu mmoja kumpenda mwingine kwa dhati kiasi mmojawapo akipata matatizo unapata hisia kama ni wewe, kujaliana kwa shida na raha. Pia kubadilishana mawazo, kuelezana undani wa familia milikotoka. 
 
Na zawadi ndogo ndogo ni miongoni mwa kachumbari ya upendo wenyewe. Kujengewa au kununuliwa gari siyo kipimo cha upendo kwani waweza ukanyang’anywa. (Mama Lulu, Kitunda Dar).
 
…Kwa maoni yangu namsihi huyu dada kitu cha kwanza kumcha Mungu. Pili, kuwa mvumilivu na kupata muda wa kumchunguza mwanaume kwani siyo kila anayemwambia anampenda akubaliane naye. (Asha Msuya wa Moshi Kilimanjaro).
Chanzo:Nipashe

No comments:

Post a Comment