Wednesday 5 March 2014

Mtoto miaka 3 adaiwa kumuua mwenzake mwenye miaka 2!!

Jeshi  la Polisi Mkoani Ruvuma linamhoji mtoto mwenye umri wa miaka mitatu mkazi wa kijiji  cha Kondowe katika kata ya Liuli, wilaya ya Nyasa kwa tuhuma za kumpiga kichwani na fimbo mtoto mwenzake mwenye umri wa miaka miwili na kumsababishia kifo.

Akizungumza  na NIPASHE mjini hapa jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Deusdediti Nsimeki alisema tukio hilo lilitokea Machi 3 mwaka huu, majira ya mchana, katika kijiji cha Kondowe.


Alisema inadaiwa siku hiyo kabla ya tukio marehemu na mwenzake anayetuhumiwa kusababisha kifo chake walikuwa wakicheza jirani na nyumba za wazazi wao.
Alieleza kuwa, Februari 27 mwaka huu majira ya saa za mchana, watoto hao  wakiwa wanacheza mtoto huyo alijeruhiwa na mwenzake kwa kupigwa kichwani kwa kutumia fimbo.

Alisema mtoto huyo baada ya kupigwa na mwenzake wazazi wake walichukulia kuwa ni jambo la kawaida kwani watoto walikuwa wanacheza hivyo hawakutoa taarifa kituo cha polisi kuhusiana na tukio hilo.

Alisema hata hivyo ghafla hali ya mtoto ilipoanza kubadilika  ndipo wazazi wake waliamua kwenda kituo kidogo cha polisi  cha Liuli kutoa taarifa ya tukio hilo na ilipofika Machi tatu mwaka huu  majira ya saa za mchana mtoto huyo  alifariki dunia.

Kamanda Nsimeki alisema polisi inaendelea kufanya uchunguzi zaidi kwa kumhoji mtoto anayedaiwa kufanya kitendo hicho, lakini  alifafanua kuwa kutokana umri mdogo wa mtuhumiwa  sheria ya makosa ya jinai chini ya umri wa miaka kumi (10) hawezi chukuliwa hatua zozote za makosa ya jinai na kwamba taratibu zinaendelea kufanyiwa kazi ili kumaliza tatizo hilo.

chanzo:Nipashe

No comments:

Post a Comment