“Niko kwenye mipango ya kutafuta mke wa kuoa licha ya kuwa hapo awali niliapa sitafanya hivyo kutokana na vitendo visivyo vya kistaarabu alivyonionyesha mke wangu niliyeachana naye kwa kuwa naona kabisa sipo sawa,” alisema Amrani.
Naye Faidha Abdul ambaye ni mama wa watoto watatu ambao alizaa bila kuolewa kutokana na kushindwana na wanaume aliozaa nao, amesema kuwa anapata wakati mgumu sana hasa kwa watoto wa kike kutokana na matendo yao kuonekana yeye anachangia kwa kuwa na yeye hana mume.
Alisema kitu hicho kinamkera sana na hutamani angeolewa hata na mwanaume mwingine achilia mbali babawa watoto hao, ili aweze kuwa angalau na stara.
“Watoto wa kike wamekuwa sasa kwani wameshamaliza elimu ya Sekondari, kibaya zaidi hawanisikii na walianza uhuni siku nyingi jambo linalonifanya nikosane na kaka yao akiamini ninafurahia, huku majirani wakinishutumu kuwa wamefuata tabia yangu ya uhuni kwa kuwa naishi bila mume. Hali hii inaninyima raha,” alilalamika Faidha.
Kwa upande wake, Silvanus Gabriel alisema kuwa alipofiwa na mkewe nusura apoteze maisha kutokana na kukumbwa na maradhi mfululizo ikiwamo kupooza.
Anasema kuwa tatizo lilianza kwa kupungua uzito bila mpangilio ghafla, baadaye alipata ugonjwa wa kiharusi uliosababisha mkono na mguu wa kushoto kuishiwa nguvu.
“Nilipokuwa kwenye mazoezi Muhimbili, nikakutana na daktari ambaye nilimfahamu kwa jina moja tu la Dk Thomas, ambapo katika maongezi ya kawaida alitaka kujua chanzo cha maradhi yangu. Nikamwambia sikuwa na tatizo zaidi ya kupungua uzito ambapo nilikuwa na kilo zaidi ya 80 nikafika kwenye 45 kwa muda mchache na sikuwa na maradhi yoyote hata homa,” alisema.
Aliongeza: “Akaniuliza tena sikuwahi kupata tatizo siku za nyuma nikamwambia hakuna zaidi ya kufiwa na mke wangu mwaka mmoja uliopita. Cha kushangaza dokta alicheka na kuniambia hilo ndiyo tatizo.”
Gabriel amesema kuwa dokta huyo alimshauri kuoa ambapo yeye mwenyewe alikuwa hataki kwa kuwa watoto wake ni wadogo akihofu watapata taabu kulelewa na mama wa kambo.
Lakini alizidi kumshauri hadi akafikia uamuzi ya kumwoa mwanamke ambaye alikuwa ni mpenzi wake baada ya kuambiwa kuwa hata kuwa na wapenzi mnaokaa mbalimbali ni tatizo pia kwani kunakuwa hakuna uaminifu.
Gabriel pia aliwashauri wanaume na wanawake wafuate taratibu ikiwamo kupima afya kabla ya kuoa au kuolewa mapema ili waweze kuongeza siku za kuishi.
Lembris anasema; “Kuna ukweli fulani na jambo hili, kuna mambo nayaelewa lakini hii si ile ambayo kila kipimo kinamhusu kila mtu (not a one size fits all kind of thing..)
Hata hivyo, asilia tumeumbwa kutegemeana mwanaume na mwanamke, mmoja akipungua kuna kitu muhimu sana kinapungua na kupata mwingine si rahisi kwa watu wengi na hasa wanawake wa Kiafrika.
“Kwa hiyo, inaeleweka lakini kama wanakufa mapema au la, nadhani utafiti unaonesha hivyo kwa ulaya zaidi - sidhani kama matokeo haya yatafanana Afrika ambamo wanawake kimsingi huishi peke yao, mume hutembelea kaya kwa zamu...yaani Afrika ya asili haina ile ukaribu wa kimapenzi kati ya mke na mume, jambo ambalo wazungu wanapenda na kuishi hivyo.
“Waafrika wanaoishi hivyo hata zamani walikufa mapema mwenzi wao akitangulia na hasa kama wameishi miaka mingi.
“Siku moja mahali fulani wenzangu wanaume walikuwa wanaongelea nyumba ndogo zao, mmoja akasema nilimwambia asionekane nyumbani kwangu mwiko. Siku moja akajitokeza nikajikausha kama simfahamu, baadae nikamfuata na kumkanya asiniaibishe!
“Nadhani hakuna kitu kizuri kama kutamba na umpendaye, ila kama mipaka na masharti yakizingatiwa, wengine yabidi kujificha, duh basi bwana uamuzi wao...mi wangu namtambulisha kila mahali mpaka aache mwenyewe! la sivyo isitokee kabisa...!
“Kuhusu nyumba ndogo, Ijapokuwa inawezekana yakawa maneno ya watu 2 tu, naamini yanatumiwa na wengi...nilihurumia jinsi yangu ya ke inayokubali kuwekwa aina hii ya mahusiano, kuwa kumbe hawa jamaa wanaitumia tu, hakuna upendo wa kweli.
Katika hali kama hii sijui kuolewa ni kupi na maisha marefu ni nini ila ubora wa maisha nadhani ndiyo jambo la msingi’,
chanzo:Nipashe
No comments:
Post a Comment