Thursday 8 May 2014

Askofu: Serikali isake wanaohatarisha amani

SIKU moja baada ya kulipuka kwa bomu katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri  Tanzania (KKKT) Usharika wa Imani, Dayosisi ya Mashariki Ziwa Victoria, Askofu wa kanisa hilo, Andrew Gulle, ameitaka serikali kutumia nguvu zake kupambana na watu wanaohatarisha amani na usalama wa nchi.
Askofu Galle alisema waliohusika na tukio hilo ni magaidi, na kwamba vyombo vya dola vinapaswa kutumia uwezo wake wote kuhakikisha matukio ya aina hiyo hayaendelei kutokea nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, alisema matukio ya kulipuliwa kwa mabomu katika nyumba za ibada, hususan za Wakristo yanaanza kushamiri, huku vyombo vya dola vikishuhudia.

Askofu Galle alisema bomu hilo lililomjeruhi vibaya mmoja wa wafanyakazi wa kanisa hilo, Bernadetha  Alfred (25), lililenga kuua watu wengi na ni ajabu kwamba halikulipuka wakati wa mkusanyiko wa watu.
Hata hivyo, alisema ingawa tukio hilo limewasikitisha na kuwaumiza waamini wengi, aliwataka watulie, wasiogope wala wasitishike na mashambulizi yaliyotendeka wala kulipiza kisasi, bali waache suala hilo lishughulikiwe na vyombo vya serikali.
“Ninatoa wito kwa Wakristo wetu wote wawe watulivu, wasiogope wala wasitishwe   na mashambulizi haya, na kusitokee fujo wala kulipiza visasi, bali sisi tuzame na kuongeza nguvu katika maombi na kumtegemea Mungu,” alisema.
Katika hatua nyingine, uchunguzi umebaini kuwa bomu hilo lililotengenezwa kienyeji, lililotegwa kanisani hapo Ijumaa wiki iliyopita, liliwekwa ndani ya bahasha na kufungwa kama zawadi na kuwekwa kwenye mfuko wa nailoni.
Imedaiwa mhudumu wa kanisa hilo, Benadetha  alichukua  mfuko huo ili  aone  kilichokuwemo, na  ndipo akalipukiwa na bomu lililomjeruhi.
chanzo:tzdaima

No comments:

Post a Comment