Thursday, 8 May 2014

Kila Mtanzania ana deni la Sh. 470,000-Ni mgawanyo wa deni la taifa la trilioni 21.2/-

Deni  la Taifa limeendelea kupaa na sasa limefikia Sh. trilioni 21.2 kiwango ambacho kama kikigawanywa kwa kila Mtanzania wanaofikia milioni 45 kwa sasa kwa usawa, kila mmoja atatakiwa kulipa Sh. 471,111.

Kiwango hicho cha deni kimepanda kutoka Sh. trilioni 16.98 cha mwaka wa fedha 2011/12.

 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, aliweka hadharani deni hilo jana wakati akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini hapa juu ya ripoti ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2012/13 ambayo inaishia Juni 30, mwaka jana. Ripoti hiyo iliwasilishwa bungeni.

Utouh alisema ongezeko hilo limesababishwa na mikopo kutoka kwenye mabenki na nchi wafadhili kwa ajili ya kusaidia miradi mikubwa ya maendeleo.

Utouh alisema deni la nje limefikia Sh. trilioni 15 hadi Juni 30, 2013  ambalo ni ongezeko la Sh. trilioni 3.0 kutoka Sh. trilioni 12.43 kwa mwaka 2011/12, wakati lile la ndani limefikia Sh. trilioni 5.78 ikiwa ni ongezeko la Sh. trilioni 1.23 kutoka Sh. trilioni 4.55 kwa mwaka 2011/12.

 “Ni maoni yangu kwamba, pamoja na deni la Taifa kuongezeka, uchumi wa nchi nao umekuwa ukiimarika kutokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali,” alisema Utouh.

MISAMAHA YA KODI
Akizungumzia misamaha ya kodi, CAG alisema ukaguzi huo umebaini kuwa hadi kufikia Juni 30, mwaka jana Sh. trilioni 1.52 zilitolewa kama misamaha ya kodi.

 Alisema mwenendo umeonyesha kuwa kiasi hicho kimepungua kutoka Sh. trilioni 1.81 mwaka 2011/12 hadi Sh. trilioni 1.52 mwaka 2012/13 ambao ni upungufu wa Sh. bilioni 290.60 (asilimia 16).

 “Hivyo naipongeza serikali kwa hatua walizochukuwa kupunguza misamaha ya kodi kwa kiasi hicho ikilinganishwa na bajeti nzima ya serikali kwa mwaka 2012/13, misamaha ya kodi ambayo ilifikia asilimia 10 ya bajeti yote,” alisema.  Alishauri serikali izidi kupunguza kasi ya misamaha ya kodi ili fedha hizo zibakie serikalini na kufanya shughuli za maendeleo.

MWENYEKITI PAC
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, alipongeza ukaguzi huo kubaini mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kunusuru fedha za walipakodi.

Alisema ripoti hiyo itaanza kufanyiwa kazi kuanzia sasa hadi Novemba ili kutoa maelekezo kwa hatua mbalimbali ambazo serikali itapashwa kuzichukua.Akizungumzia misamaha ya kodi, Zitto, alisema pamoja na kupunguza kiasi hicho hadi kufikia asilimia tatu ya pato la taifa, lakini bado ni kikubwa na kushauri ifikie asilimia moja ya pato la taifa.

Alisema wanakusudia kuwasilisha muswada wa mfumo mpya wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat) wenye lengo la kudhibiti misamaha ya kodi, ambao alisema unapigwa vita na baadhi ya wabunge na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wa madini.

 HATI CHAFU
Utouh alisema serikali imetoa hati za ukaguzi 961 kati ya hizo, 131 zimetiliwa shaka wakati nane zikiwa haziridhishi na mbaya zikiwa sita.

Alisema ukaguzi huo ulifanywa kwa halmashauri 140, wizara na idara na taasisi za serikali 117, mashirika na taasisi za umma 93, miradi ya wafadhili 611 na kubaini kasoro hizo.

Alisema pamoja na kuwapo kwa hati hizo chafu na zisizoridhisha, mwelekeo wa hati za ukaguzi kwa ujumla unaonyesha kuimarika kwa utendaji wa serikali katika kusimamia makusanyo ya mapato na matumizi ya rasilimali za umma ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Alisema katika wizara na Idara za Serikali zilikuwa 117 na kuwa walibaini hati 85 zinaridhisha, hati 30 zenye mashaka, hati isiyoridhisha ilikuwa moja na hati mbaya moja.

Kwa upande wa halmashauri, alisema zilikaguliwa 140 na kubaini hati zinazoridhisha 112, zenye mashaka 27, isiyoridhisha bila kuwapo mbaya wakati. Kwenye mashirika ya umma taasisi zilizokaguliwa zilikuwa 93 hati zinazoridhisha zilikuwa 92, yenye shaka moja, hakukuwa na hati siyoridhisha wala mbaya.

 Katika miradi ya wafadhili iliyokaguliwa ni 611 na kupata hati zinazoridhisha 527, zenye shaka 73, zisizoridhisha sita na mbaya tano.

 Alisema hati zenye shaka kwa upande wa serikali kuu zimeongezeka kutoka tano mwaka 2011/12 hadi kufikia 30 mwaka 2012/13 kiliwango ambacho kimeongezeka mara tano.
Alizitaja sababu za ongezeko hilo kuwa ni uandaaji wa hesabu kwa kufuata mfumo mpya wa viwango vya kimataifa vya uhasibu (IPSAS-Accrual) ambao unaotambua madeni na mali za kudumu zinazomilikuwa na serikali kitu ambacho kilikuwa hakifanyiki miaka ya nyuma.

Kwa upande wa halmashauri, Utouh, alisema hati zinazoridhisha zimeongezeka kutoka asilimia 78 hadi 80 kwa mwaka uliopita wakati mashirika ya umma hati zinazoridhisha zimeongezeka kutoka asilimia 90 hadi 99 na ripoti za wafadhili hati zinazoridhisha zimeongezeka kutoka asilimia 81 hadi 86.

Alisema jumla ya mapendekezo 102 aliyotoa kwa serikali 22 yalifanyiwa kazi kikamilifu wakati 57 yanaendelea kufanyiwa kazi huku 23 utekelezaji wake upo katika hatua ya awali.

WATUMISHI HEWA

Katika hatua nyingine, CAG utouh alisema kwamba ofisi yake imebaini kuwapo kwa watumishi hewa wanaolipwa mabilioni ya fedha.

Watumishi hao inadaiwa ama wameacha kazi au wamekufa na jumla ya malipo yao kama mishahara yalifikia Sh. bilioni 1.62 huku makato mengine yakifikia Sh. milioni 497 katika kipindi cha mwaka wa fedha unaoishi Juni 30, mwaka jana.

Utouh alisema makato hayo yalikatwa katika mishahara hiyo na kupelekwa katika mifuko mbalimbali ya jamii.

Kutokana na hali hiyo, alishauri Serikali kuzifuatilia fedha hizo zilizolipwa isivyo halali kutoka kwa mifuko ya hifadhi ya jamii, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bima ya Afya.

Akizungumzia kuhusu mali na fedha zisizo na mwenyewe, Utouh alisema ukaguzi umebaini kuwa katika taasisi za fedha na mifuko ya jamii kuna fedha ambazo zinakaa muda mrefu bila kuchukuliwa na wenyewe kutokana na sababu mbalimbali kama vile kufariki dunia, makato ya kisheria kwa wafanyakazi walioachishwa kazi au kustaafu.

Alisema Hazina wamekuwa wakiendelea kupeleka makato hayo katika mifuko hiyo, amana ambazo zimetelekezwa na wenyewe kutokana na uchache wake, fedha za mirathi, fedha haramu na gawio zisizo chukuliwa.

“Katika nchi mbalimbali kuna sheria zinazozitaka taasisi zinazojikuta zina fedha kama hizo kutakiwa kuzipeleka katika mfuko maalum unaotunzwa na Hazina,” alisema na kuongeza:

“Fedha hizo huwa zinatunzwa kwenye mfuko huo kwa kipindi maalum kabla hazijatumiwa kwa ajili ya maendeleo ya jamii. Endapo mwenyewe fedha hizo atajitokeza na vielelezo vinavyothibitisha uhalali wa madai yake mfuko utamrejeshea kiasi anachostahili kulipwa.”

Hata hivyo katika ukaguzi huo ilibainika jumla ya magari 11 kwenye Wizara ya Viwanda na Biashara yamenunuliwa yakiwa mapya, lakini hadi leo hayajulikani yalipo.

Utouh alisema suala hilo hawezi kulizungumzia kwa undani zaidi kwa vile liko mikononi mwa taasisi nyingine za kisheria kwa ajili ya ufuatiliaji.

Zitto alisema ili kudhibiti fedha chafu na mali ambazo hazina mwenyewe kuna haja kwa Serikali kuanzisha chombo maalum kwa ajili ya kuzisimamia ikiwezekana baada ya kipindi maalum zipangiwe utaratibu mwingine.

VYAMA SITA HAVINA AKAUNTI
Wakati huo huo, Utouh alisema kuwa vyama vinne vya siasa vyenye usajili wa kudumu havina akaunti ya benki wala watalaam wa mahesabu.

Alivitaja vyama hivyo kuwa ni UMD, NLD, NDC na NRA ambavyo licha ya kufanya shughuli mbalimbali za kisiasa kwa kutumia fedha za michango ya wanachama wao, lakini hazina udhibiti wowote.

Alisema kuwa pamoja Serikali kutoa ruzuku kwa baadhi ya vyama vyenye wabunge, lakini navyo vimekuwa vigumu kukaguliwa huku baadhi yake havina watalaam wa mahesabu.

Alisema vyama vya siasa 11 kati ya 21 vyenye usajili wa kudumu havikuwasilisha hesabu za mwaka kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa namba tano ya mwaka 1992.Utouh alisema taarifa za mahesabu zilizowasilishwa na vyama hivyo hazikufuata misingi ya uhasibu na mfumo wa utoaji wa taarifa za fedha wa kimataifa.

Hata hivyo, alisema hesabu za vyama vya siasa saba vilivyokaguliwa hazionyeshi mali za kudumu na za muda mfupi zinazomilikiwa na vyama hivyo na kusababisha ukaguzi wake kuwa mgumu.

Alishauri kuwa ili kuboresha utoaji wa taarifa, uwasilishwaji na ulinganifu wa utendaji wa vyama vya siasa, anapendekeza kuwa vyama viandae taarifa za hesabu kwa mujibu wa viwango vya kihasibu vya kimataifa.

“Msajili wa vyama vya siasa akishirikiana na mhasibu mkuu wa Serikali watoe mwongozo, aina ya mfumo na muundo wa taarifa za fedha utakaotumiwa na vyama vya siasa,” alisema Utouh.
chanzo:Nipashe

No comments:

Post a Comment