Monday 14 July 2014

Uhausigeli ulinitega nusura niuzwe Uarabuni!

Kwa nchi yetu tatizo hili japokuwa halitiliwi uzito mkubwa lakini lipo linafanyika chini kwa chini na vijana wetu hasa watoto wa kike ndiyo waathirika wakubwa. Ipo biashara iliyozoeleka ya msichana kutolewa kwa wazazi wake kutoka mkoa mmoja hadi mwingine.

Hawa ndiyo tunaowaita wadada wa nyumbani(hausigeli). Nauli itatumishwa kwa wazazi wake na kisha binti atasafirishwa hadi kwa yule tajiri anayemhitaji kumfanyia kazi. Hili ni kundi moja ambalo wengi wanalitumia kuwafanyia kazi za majumbani.

Lakini lipo kundi lingine la wasichana wanaoagizwa toka mikoani na kisha kuwarundika katika madanguro kwa kuwauza kwa wanaume (ukahaba) na huyo anayewamiliki hujipatia fedha nyingi zilizojaa laana na dhambi ya mauti. 


Kundi lingine la mabinti ambalo ndilo nataka kulizungumzia hapa ni lile la mabinti wanaochukuliwa kama mahausigeli majumbani kisha baadaye wanarubuniwa kupelekwa ulaya kumbe huko nako wanakwenda kufanyishwa kazi za suluba ikiwa ni pamoja na biashara ya ngono. Hebu sikia mfano huu halisi wa kilichomtokea binti huyu.

Nikawa nahojiana naye kwanini aliondoka kwenye familia hiyo kisha kurudi kijijini ambako ndiko alikotokea na kuja hapa Dar. Anasimulia hivi;-

“Mimi nilikuwa nafanya kazi za nyumbani katika familia ya kiarabu. Ni familia ya watu watano.  Wafanyakazi tulikuwa wanne, wasichana wawili na wavulana wawili na kila mmoja alikuwa analipwa mshahara wa sh.70,000/- kwa mwezi.

Tulikuwa tunakula vizuri, kuvaa bila tatizo. Kazi yangu mimi ilikuwa kupika wengine walikuwa wakifanya usafi, kufua na kadhalika. Familia hii ilikuwa na watoto watatu ambapo wa mwisho alikuwa darasa la tano.

Nimekaa na familia hii kwa muda wa miaka miwili. Haina tatizo. Ila lipo jambo moja lililoniogopesha na ndilo lililonifanya nifungashe virago nirudi kwetu kijijini yasije yakanikuta makubwa.

Siku moja mama tajiri yangu nilimsikia akiongea kwenye simu na mazungumzo yakawa yanaonyesha kama wanaulizana kuhusu idadi ya wafanyakazi wa kike walio nao. 

Yule mama tajiri yangu akamwambia yeye anao wawili kwa sana kwani yule wa tatu alishapelekwa kwenda Nairobi. 

Na mwenzake kwenye simu akamwambia yeye anao wawili na bado anasaka wengine kabla ya kuwapeleka uarabuni. Mazungumzo haya yaliniogopesha sana nikawaza inawezekana tunakusanywa kwa lengo fulani.

 Yule binti aliyepelekwa Nairobi alikuwa na simu lakini tangu aondoke hajawahi kuwasiliana na sisi wala wazazi wake kijijini na haijulikani yuko katika hali gani.

Hofu iliniingia zaidi pale familia ile ilipotukusanya siku moja jioni na kutuambia kuwa wao wanataka kusafiri kwenda Uarabuni na lazima na sisi wafanyakazi wote tuondoke nao. 

Waliposema vile, mimi nikakumbuka yale mazungumzo ya simu wakiulizana idadi ya wasichana walionao.  Ndipo nilipompigia mama yangu simu kijijini na kumjulisha kuhusu mazungumzo yale ya simu na pia mpango wa kutupeleka uarabuni. 

Mama yangu akaniambia nisikubali niwaambie kwamba lazima nirudi nyumbani nikawaage wazazi kisha ndipo nifuatane nao kwenda uarabuni. 

Baada ya kuelewana na mama yangu nikamfuata mama tajiri yangu nikamwambia kuwa mama mzazi ananihitaji nyumbani kwanza kabla ya kwenda huko uarabuni.

Mungu ni mkubwa wakanikubalia kuondoka na ndipo waliponiandalia safari pamoja na kunilipa mshahara wangu na zawadi tele kwa ajili ya familia. Pia walinikatia tiketi ya basi nikaondoka zangu.

Nilimshukuru Mungu kwani sikutarajia tena kurudi kwenda familia ile. Tangu wakati huo mama yule amekuwa akinipigia simu kuniulizia ni lini narudi kwani wamenimisi sana. Nami humwambia najiandaa nitakuja tu (kumbe hawataniona tena).

Hata jana (Jumatano) mama huyo alinipigia simu akiniambia kuwa nimwelekeze kijijini kwangu atakuja na gari lake kunichukua nami nikamjibu asiwe na wasiwasi nitakuja tu, kumbe sina mpango. 

Na baada ya mimi kuondoka, hata yule binti mwingine naye aliondoka pamoja na vijana wale wawili na sasa nimeambiwa na huyo mwenzangu aliyeondoka kuwa ameletwa msichana mwingine mgeni”, anamaliza kueleza binti huyu.

Mpenzi msomaji wangu, hayo ndiyo maelezo ya binti ambayo yamenifurahisha sana na zaidi nikionyeshwa kuwa Mungu wake amempa Roho Mtakatifu mwema amwongozaye na Malaika mlinzi anayemlinda dhidi ya maadui zake.

Mazungumzo yale ya simu ndiyo yaliyomwokoa binti vinginevyo angeweza kujikuta katika mazingira magumu kimaisha kuliko ambavyo angeweza kufikiria. Ama kweli Maisha Ndivyo Yalivyo.

Inaonekana dhahiri familia ile ina mchezo mchafu wa kuwasafirisha wafanyakazi wao kwenda nje kwa shughuli maalum. 

Kwanini waulizane kuhusu idadi ya wasichana waliona? Siyo siri kwamba biashara ya binadamu imeshamiri sana sehemu mbalimbali duniani ikiwamo Tanzania na huko uarabuni. 

Mabinti wanachukuliwa Afrika na kwenda kuuzwa kwa watu ambao nao huwatumikisha katika biashara chafu hasa ukahaba.  

Kwa mujibu gazeti la Mwananchi la hapa nchini, Marekani ilitoa ripoti inayozungumzia usafirishaji wa binadamu ya mwaka 2013, huku ikiitaja Tanzania kuwa kinara wa kunyanyasa wasichana, kuwatumikisha katika ngono na usafirishaji wa binadamu.

Ripoti hiyo iliyotolewa na idara ya nchi hiyo inayohusika na diplomasia (US Department of State, Diplomacy in Action), pia inaitaja Tanzania kuwa ni kitovu cha njia ya kusafirisha wanawake, watoto na wanaume ambao hutumikishwa kwenye kazi za mashambani na biashara ya ngono.

Ripoti hiyo iliyozinduliwa Julai  mwaka huo   na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Seneta John Kerry inaweka bayana kwamba biashara ya usafirishaji wa binadamu hufanywa na baadhi ya ndugu na marafiki ambao hutoa ahadi kwa wahusika kwamba wanakwenda kuwasomesha au kuwatafutia ajira nzuri mijini.

“Unyonyaji wa wasichana wadogo na utumikishaji majumbani ndilo tatizo linaloongoza, ingawa kesi za watoto kusafirishwa kwa ajili ya biashara ya ngono katika mpaka wa Tanzania na Kenya zinaongezeka. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto kutoka Burundi na Kenya, watu wazima kutoka Bangladesh, Nepal, Yemen na India wanatumikishwa kufanya kazi kwenye sekta za kilimo, madini na majumbani nchini Tanzania.

Ripoti hiyo inaitupia lawama Tanzania kwa kutokuwa na sheria thabiti za kupambana na biashara haramu ya kusafirisha binadamu, huku ikitolea mfano namna ilivyoshindwa kuwasaidia raia wake waliokuwa wakinyanyaswa nje ya nchi.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment