Wednesday 19 November 2014

Mke wangu ana kipato, matumizi natoa mimi tu kwanini

 

Mke akitoa hela ya chakula siku moja tu majirani watajua na kasheshe siku akiachwa hata kucha zinakonda na kwa waganga juu. (namba yangu kapuni).

Mpenzi msomaji, ndugu yetu huyu ambaye kwa maelezo haya ni baba, anataka kujua, iweje wote mke na mume wana kipato lakini mmoja anabana kuchangia mahitaji ya familia?

Swali hili limenikumbusha wimbo fulani sikumbuki vizuri mtunzi wake kwani ni zamani sana ambao ulikuwa na maneno yafuatayo; …changu chako wewe, chako chako weweeeee!

Labda tu niseme kwamba kwa mke na mume linapokuja suala la kuchangia kipato, inaeleweka kabisa endapo mmoja anakuwa na uwezo mdogo huku mwingine akiwa na uwezo mkubwa. Kama mama ni wa nyumbani, hana kazi inayomwingizia kipato na baba ni mfanyakazi au mjasiriamali, vyovyote vile baba ndiye atakuwa tegemeo kubwa.

Lakini pale inapotokea wote, baba na mama ni watafutaji, wana miradi au ni wafanyakazi maofisini, hawana budi kila mmoja kuona umuhimu wa kuchangia matumizi ya familia yao. Maisha Ndivyo Yalivyo.

Familia nyingi zenye uelewa mpana, ambao baba na mama wote ni wenye kipato, wamejiwekea utaratibu wa kuchangia; mfano kama baba analipa ada za watoto shule, mama yeye anaweza kwa kiasi fulani kununua mahitaji ya chakula na pengine nguo za wanafamilia kwa maana ya watoto na kadhalika. Zipo familia ambazo zimejipanga kwa jinsi hiyo na zinaishi vizuri sana.

Hata hivyo, wapo wengine ambao pamoja na kupenda kuchangia, mfano mke, hukatishwa tamaa pale anapogundua kuwa mumewe anabania matumizi ya familia lakini anachepusha pembe za chaki (hawara au kwenye ulevi na kadhalika).

Na mume pia anaweza kuzidiwa, tuseme kipato kimeshuka na wakati huo huo akitegemea mkewe ataokoa jahazi, lakini anajikuta akipata upinzani kwa mama kukatalia kipato chake, tena kwa kebehi tele. Na je, kama mama ana kipato na hachangii matumizi, fedha zake huishia wapi?

Ushugamami? Miradi ya siri?
Baba huyu aliyeuliza swali hapo juu kuhusu kwanini mke anapotoa matumizi ya familia anajigamba mtaani, hiyo siyo sahihi kabisa. Zipo sababu nyingi ninazoweza kuzieleza hapa, ila nitajaribu kueleza chache.

Kwanza kikubwa hapa ndoa ni kusaidiana. Unaposimama madhabahuni na kuahidi kumpenda mwenzio kwa shida na raha, tena hadi kifo kiwatenganishe siyo tamko la kuchukuliwa kimzaha mzaha hata kidogo.

Hata Mungu wetu ni Mungu wa ahadi na anasisitiza kuwa kile alichoahidi ni lazima kitatimia. Na ahadi tunazotamka wanadamu tusichukulie ni utani kwani tayari tamko hilo limeshaandishwa kwenye ulimwengu wa roho.

Ndoa ni mapatano ya mtu zaidi ya mmoja. Mke, mume, kiongozi wa ndoa, washenga na watu wote walioshuhudia ndoa hiyo ikifungwa. Na mapatano hayo yanapovunjika hushangaza. Mjadala huu ni mrefu.

Turudi kwenye kipato cha mke na mume kitumikeje. Mtuma ujumbe anauliza kwa nini  mke akitoa matumizi anatamba mtaani yaani kila mtu atajua. Hii siyo sahihi.

Nadhani angeona fahari kwamba hata yeye anaihudumia familia yake kutokana na pato lake. Pia angeona fahari kumsaidia mumewe kutunza familia.

Maisha ya ndoa yana kanuni mbalimbali zinazoilinda na zikizingatiwa hakuna migogoro ya aina yoyote. Wengi wanaozikiuka kanuni hizi kwa kuzijua au kwa kutozijua, ndio hao ambao kika kukicha ndoa zao zinatikisika na wakati mwingine kuvunjika kabisa.

Kanuni hizi ni pamoja na; Kufanya majadiliano. Njia nzuri ya kushughulikia matatizo ni kufanya majadiliano.

Kuacha kufungua ukweli na kukubali kukaa pamoja na kujadilia matatizo, maana yake ni kukaribisha matatizo zaidi. Wanandoa wengi wamejikuta wakiingia kwenye malumbano kwa sababu ya kutokubali kukaa pamoja na kumaliza kasoro zao.

Hakikisha unafanya kila linalowezekana kuwa mbali na kukaribisha matatizo, na kama itatokea ukashindwa kuelewana na mwenzako, basi njia nzuri ni kukaa pamoja na kuyaongea.

Wengine wana tabia ya kupuuza tatizo wakidhani matatizo makubwa tu ndiyo yanayopaswa kuangalia. Uzoefu unaonyesha kuwa matatizo madogo kwenye mahusiano ndani ya familia yasiposhughulikiwa mapema ndiyo ambayo baadaye huzaa matatizo makubwa.

Kuvumiliana na eneo lingine linahitaji mtizamo wa karibu ili ndoa idumu. Mahali pasipo na uvumilivu, maana yake hakuna upendo. Usione udhaifu wa mke au mume wako kuwa ni mzigo wake mwenyewe, lakini badala yake uwe tayari kuubeba pamoja. Kwenye ndoa wanasema, wapenzi wanapaswa kuishi kuvumiliana kwa kila jambo kwa vile wao ni wamoja kwa kila jambo.

Umoja umesisitizwa pia katika maandiko ya Mungu. Hebu sikia Bwana Yesu anavyosema katika maandiko ndani ya Biblia Takatifu; Yohana 17:22-23 kuwa; nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa wewe ndiwe uliyenituma ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi.

Hapa msisitizo ni UMOJA na UPENDO. Wakati ukimvumilia mwenzako, hakikisha upendo na umoja vinakuwa ndio msingi mkuu wa kurekebishana.

Zipo kanuni nyingi kama vile udhaifu kwenye ndoa, kuheshimiana ambavyo vinapaswa kupewa kipaumbele katika maisha ya wawili wapendanao.

Kwa leo niishie hapa tupate maoni zaidi toka kwako msomaji wangu kuhusu kipato chako na mkeo…ushirikiano katika pato kwa matumizi ya familia ukoje?
 
chanzo: nipashe

No comments:

Post a Comment