Friday 18 January 2013

DC atangaza gesi imezua balaa Mtwara

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mjini, Wilman Ndile, amesema suala la gesi kwa sasa ni tishio kubwa kwa amani na utulivu kwa wakazi wa Wilaya na Mkoa wa Mtwara.

Kutokana na hali hiyo, amewataka viongozi wa asasi mbalimbali mkoani hapa kutoa elimu kuhusu gesi asilia kwa wakazi wake ili kudumisha hali ya amani na utulivu, ambavyo vinaelekea kutoweka siku hadi siku.

Alitoa kauli hiyo alipokuwa akitoa hotuba yake fupi kwenye kikao cha Baraza la Madiwani Mjini Mtwara.

Alisema kwa sasa hali ya Wilaya ya Mtwara kiusalama, kisiasa na kiuchumi siyo nzuri kutokana na suala la gesi, ambalo limekuwa gumzo kila kona ya mkoa na kutishia kutoweka kwa amani na usalama.

“Kwa kweli hali iliyopo hivi sasa Mtwara siyo nzuri kiusalama. Kwani inaweza kuhatarisha maisha ya Wanamtwara. Sijui tunakoelekea. Maana kila kona unakopita hakuna mazungumzo mengine zaidi ya gesi ikiambatana na kauli mbiu yao ya ‘gesi kwanza vyama baadaye’,” alisema Ndile na kuongeza:

“Hii ni mbaya na ni hatari, kwani suala hili linaweza kuleta madhara makubwa katika siku za usoni.”

Alisema ni lazima kutenga muda maalum kwa ajili ya kuwaelimisha watu ili wapate uelewa na kutambua manufaa yatakayotokana na rasilimali hiyo na kwamba bila kufanya hivyo, hali ya utulivu na usalama haiwezi kuwapo.

“Wanamtwara ni waelewa wazuri tu endapo wataelimishwa kwa lugha iliyokuwa nyepesi na 
elimu badala ya ubabe,” alisema Ndile.

Alisema ni lazima kufanya kila linalowezekana kutenga muda maalum wa kufanya mazungumzo kati ya viongozi na wananchi ili kuweka mambo sawa.

Hata hivyo, utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya masuala ya gesi utaanza mapema wiki ijayo kwa lengo la kurejesha hali ya amani na utulivu.

Pia alisema suluhisho la suala hilo lipo katika mikono ya serikali kwani cha msingi ni kupata suluhu ya tatizo hilo ili kuiondoa jamii mahali ilipo na kurudisha imani dhidi ya viongozi wao.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment