Geita. Mtoto mchanga mwenye umri wa miezi minne amezua kizaazaa cha aina yake, baada ya kuwapo taarifa kwamba mara kadhaa umbo lake limekuwa likigeuka na kuwa nyoka na mwili wake ukiendelea kudhoofu kutokana na kukataa kunyonya maziwa ya mama yake.
Mtoto huyo (jina lake tunalihifadhi kwa sasa), wiki iliyopita alivuta umati wa wakazi wa Kijiji cha Nkome mkoani Geita ambao walifurika ndani na nje ya Kanisa la AICT Nkome, lililopo kijiji hapo, kushuhudia maombi ambayo alikuwa akifanyiwa ili kumkomboa katika kile kilichotafsiriwa kuwa ni mateso dhidi yake.
Ilikuwa saa 4.00 asubuhi Jumamosi, Novemba 8 mwaka huu wakati mtoto huyo alipofikishwa katika kanisa hilo na kuanza kufanyiwa maombi na sababu ya hatua hiyo ikielezwa kuwa ni kutokana na kuwa na umbo la nyoka na kwamba matendo yake yanaashiria kwamba mwenye asili ya nyoka ndani ya roho yake.
Mtoto huyo alifikishwa kanisani hapo na mama yake mzazi, Sarah Silasi wakitokea Kijiji cha Ichile, Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, ambako alikimbia matukio yanayohusishwa na ushirikina.
Mmoja wa wazee wa kanisa hilo la AIC Nkome, Mathew Misana anasema: “Alikuwa anatoa ulimi mithili ya nyoka, mwendo wake anapolala alijizungusha kama nyoka na hata alipojikunja mwili wake ulikuwa kama unavyoona nyoka.”
Misana anasema matukio hayo na mengine kadhaa yakiwamo ya ngozi ya mtoto huyo kuwa nyeusi kama ya nyoka aina ya chatu, yaliwalazimisha ndugu na jamaa zake wakiongozwa na mama mzazi kutaka aombewe.
“Ngozi yake kuonekana kama ya mzee huku macho yake yakionekana kuwa makubwa na kichwa chake kuwa na umbo la nyoka pamoja na miguu, baada ya kuona hali hii tukaihusisha na mambo ya kishirikina na kuamua kuanza maombi,” alisisitiza.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya maombi kuanza, taarifa za kuwapo kwa aina hiyo ya mtoto zilisambaa haraka na kusababisha umati mkubwa wa watu kujaa ndani ya kanisa hilo ambalo ni boma kwa maana kwamba ujenzi wake bado unaendelea.
“Watu wengi walijaa na wengine wakawa wanapanda juu ya miti na juu ya boma wakati mwingine matofali yalianguka. Hewa ikapungua na usalama ukawa mdogo kwani watu walisukumana wakitaka kushuhudia,” anasema Misana.
Baada ya watu kuwa wengi, uongozi wa kanisa uliomba msaada wa Polisi wa Kituo cha Nkome ambao walifika kanisani hapo na kushauri mtoto huyo aonyeshwe ili watu waweze kuridhika kwamba hakuwa amegeuka kuwa nyoka.
Uongozi wa kanisa ulifanya hivyo lakini mwonekano wa mtoto huyo ulisababisha watu kuongezeka badala ya kupungua na hapo ndipo polisi walipoelekeza mama wa mtoto huyo ambebe na kuondoka naye hadi kituoni.
Mwinjilisti wa kanisa hilo, Emmanuel Misungwi anasimulia: “Tumeshudia vitu visivyo vya kawaida wakati tunafanya maombi na wakati tunaendelea na huduma, mama wa mtoto Sarah alianguka akaanza kuongea juu ya mtoto kwa nguvu ya mapepo.”
chanzo:mwananchi
No comments:
Post a Comment