Monday, 5 January 2015

Talaka iko mlangoni, unakumbuka shuka asubuhi!



Iko hivi; yupo kijana ambaye ameishi na mkewe hadi kubahatika kuzaa watoto wawili. Kijana ni mjasiriamali wakati mkewe huyo ni mama wa nyumbani. Baada ya kuzaa watoto hao, kijana akaomba ridhaa ya wazazi wake wafunge ndoa na mama watoto wake.

Wakakubaliwa wakafanya maandalizi. Zikatangazwa zile ndoa za mwisho wa mwaka ambapo wapendanao huambiwa wajiandikishe, wajinunulie pete na kwenda kufunga ndoa za watu wengi. 

Hizi ndoa wengine huita ‘za mafungu’, ‘vipasha kiporo’ kwa sababu miongoni mwana wapo walikwisha kupata watoto.

Kijana huyo na mama watoto wake wakafunga ndoa. Mwanzoni hali ilikuwa shwari lakini baada ya muda mwanamke yule akaanza kuonyesha makucha yake, akaanza kumnyanyasa mumewe. 

Watoto wao ni wadogo, wa kwanza  darasa la kwanza na wa pili bado hajaanza. Mume huyu kila mwezi humpa mkewe Sh. 200,000/- za matumizi ya nyumbani mbali na ada ya mtoto shuleni.

Lakini cha ajabu, mwanamke huyu hatulii nyumbani na mara nyingi huwapeleka watoto kwa mashoga zake na pia ni hodari sana kwenda kwa waganga wa kienyeji. Mashoga zake nao ndiyo njia moja kiguu na njia kwa waganga eti kuwaweka sawa waume zao wasifurukute.

Na kibaya zaidi, wamekuwa wakiwapumbaza waume zao ili waweze kwenda kujinafasi sehemu za starehe. Kwa kifupi mwana mama huyo siyo mleaji bali ni mzururaji. 

Hakuweza kujitambua kuwa anaye mume mzuri, mpole na mchakarikaji kwa ajili ya kuinua maisha ya familia yake.

Unajua mwanamke anapoujua udhaifu wa mumewe, kumuonea ni dhahiri. Wapo wanaume ambao huwapenda wake zao kiasi cha kujisahau. 

Na wanawake wa aina hii wanapobaini kuwa wanapendwa sana, badala ya kuonyesha upendo zaidi, wao ndio kwanza huichukua hiyo hali kama silaha ya kuwaumiza wanaume zao.

Hii Mwenyezi Mungu aliiona mapema hata kabla ya kuumbwa ulimwengu na kupitia Mitume na Manabii wake aliweka tahadhari kwa wanaume pale aliposema kwenye maandiko yake; Mithali 7:11-12 neno linasema… Alikuwa mwanamke wa makelele na mkaidi; miguu yake haitulii nyumbani. Mara barabarani, mara sokoni, katika kila kona ya njia hakosekani akivizia.

Katika Biblia habari njema kwa watu wote yenye vitabu vya Deuterokanoni kitabu cha Hekima ya Yoshua mwana wa Sira sura ya 9:2 neno linasema; Usimwachie mwanamke ukuu wako, la sivyo atakutawala kabisa.

Mpenzi msomaji, wanawake wengi ambao waume zao waliwaonyesha upendo wa hali ya juu, ndiyo hao wamekuwa wasaliti wakubwa kama mwanamama ninayemchambua katika makala haya.

Huyu hakutaka kutulia hata pale mumewe alipotaka afanye shughuli fulani ya kuingiza kipato alikataa, lakini kiguu na njia kwa waganga na kwenye maeneo ya starehe alikuwa hodari. 

Huyu alisahau kuwa nguvu za giza anazotafuta kwa waganga huwa zinachujuka kama tui la nazi na kuisha ladha yake kisha yanafuata madhara.

Mungu wa rehema akaingilia kati  kumuokoa kijana huyo katika mateso yaliyokuwa yakimsibu kila kukicha. 

Mwanamke hampikii chakula cha maana, hamfulii nguo lakini yeye kila wakati anakwenda saluni kujipendezesha, tena kwa fedha alizopewa na mumewe. Mume akiugua anamnyanyapaa, eti ananuka, eti aende kwa wazazi wake wakamhudumie na maudhi kibao.

Mume akiugua huwaita wazazi na ndugu zake waje wamchukue kumpeleka hospitali. Vikao vikaitishwa mara kadhaa kumuonya ikashindikana. Mwanamama huyo akaomba msamaha hadi kupiga magoti lakini baada ya kuondoka hapo akacharuka mara mbili. 

Kijana kuona yamemshinda akapeleka mashtaka ustawi wa jamii ambako nako wakasuluhisha lakini ikaonekana shauri hilo yafaa liamuliwe kimahakama. Kijana akafungua kesi ya talaka.

Sasa yamemfika maji ya shingo, mwanamama anatapatapa kila tawi analolishika linakwanyuka hakuna awezaye kumsaidia. Laiti angelijua andiko hili; Mithali 14:1  neno la Mungu linasema; Mwanamke mwenye hekima hujenga nyumba yake, lakini mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.

Mpenzi msomaji, yapo mambo mengi wanadamu tunayafanya kwa pupa pasipo kutafakari yanayokuja siku za usoni. 

Tunayawazia ya leo, tunasahau pia ipo siku nyingine kwa majaliwa ya Mwenyezi Mungu.

Kama umebomoa nyumba yako mwenyewe na tena baada ya kuonywa mara kadhaa pasipo kubadilika, unategemea nani atakuokoa? Utashangaa hata wale wapambe waliokuwa wanakuchochea kufanya maasi wanakutosa kwani unakuwa mzigo kwao.

Maajenti wa ibilisi ni wengi. Tena watakushawishi mambo mengi, kisha ukishayatenda, wanakaa pembeni wakikutizama unavyohangaika. 

Shetani kazi yake ni kushawishi , kuharibu na kuua. Ukishakubaliana na ushawishi wake anakaa mbali nawe. 

Sasa talaka iko mlangoni, wewe ndiyo kwanza unakumbuka shuka wakati tayari ni asubuhi. Mwanamke jitambue, unapopewa mji wake, usikubali mwingiliano na sauti za ushawishi za nje. Mungu akikupa mume/mke tulizana na kisha maombi yawe ndiyo silaha kuu katika maisha ya ndoa yenu.

Angalia Biblia kitabu cha Matendo 7:7-8  Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtaona; bisheni nanyi mtafunguliwa  kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. 

Tena lipo andiko linalofanana na hili lisemalo ombeni nanyi mtapewa ili furaha yetu iwe timilifu.

Hakuna kitu ambacho utamuomba Mungu na kuamini kwa dhati ya moyo wako usikipate. Wewe amini tu, vyote vitakamilishwa kwa maana Mungu wetu ni Mungu wa ahadi na hakuna alichokiahidi ambacho hatakitimiza juu ya maisha yako
.

Matatizo mengi ndani ya familia zetu chanzo chake ni sisi wenyewe. Ni muhimu tuyashinde kwa kutimiza wajibu na kanuni za kimaisha ikiwamo upendo, heshima, utii na uvumilivu

chanzo:nipashe


No comments:

Post a Comment