Monday, 26 January 2015

Unapochagua mchumba tulia, usijeokota kanyaboya!

Ndugu yangu huyu nampa pole sana, kwa upande mmoja maisha yaliompitia yanafanana na yangu, kapitia uyatima, ambao na mimi nimeupitia nikiwa na umri wa miaka 9, wakati baba yangu mzazi alipouliwa na majambazi.

Sikuwahi kuitwa mtoto wa mitaani bali sikuwa mbali sana na jina hilo, kwani niliwahi kulala nje, kuishi katika kibanda kibovu na kulala katika uchaga kwa miezi fulani, huku ikiwa godoro ni majani makavu ya mgomba na kitambaa ni gunia, chakula ni sembe, mihogo na papa mchungu.

Cha kusikitisha sana, nilikuwa na watu wa karibu ambao wangeweza kunisaidia bali walikataa. Nimesoma hadi kufikia sekondari lakini kwa shida tupu.


Hata hivyo, baada ya dhiki si dhiki ilinichukua miaka 18 tokea kufa baba yangu mpaka kufaulu na maisha, na wakati wote ndoto yangu ilikuwa nifanikiwe na maisha niwalipe mema wale walonifanyia ubaya na niwazidishie wema wale walonifadhili. Kwa uwezo wa Mola wetu ndoto yangu nimefanikiwa.

Tukirudi kwenye mada yetu namshauri ndugu yangu huyu, atafute njia ya kujinasua na mateso haya.

Njia moja ambayo itasaidia awatafute watu wenye busara, kiitishwe kikao cha familia ya mama mtoto wake.

Nafahamu fika mwanaume si wa kukaa nyumbani na kuchombeza mtoto bila ya kumtafutia chakula kwa jasho lake.

Ikishindikana aende kwenye taasisi za dini ili apewe nasaha mama mtoto wake, kuwa ajue baada ya maisha haya ya duniani kuna maisha mengine ya akhera na mlipaji hapendelei na malipo ya huko zuri kwa zuri na baya malipo yake ni moto.

Ahsanteni. Wenu mzee Salum, Zanzibar.
…Mwingine anasema kwenye ujumbe wake simu ya kiganjani yafuatayo; Rejea tatizo la kijana katika safu ya Maisha Ndivyo Yalivyo, kwanza aanze kujiamini aelewe kwamba wanaume ndiye kichwa cha familia na tegemeo.

Endapo ataendelea kukubali kubaki nyumbani akilea na kumwacha mwanamke aende kazini, hatakuwa na maendeleo na familia itaishia kuwa masikini.
Matokeo yake yeye ataishia kulaumiwa kwa hilo.

 Huyo mtoto naye atamlaumu pia. Hivyo anapaswa kuwaelewesha mke na wakweze juu ya athari za yeye kuacha jukumu la kuwa mtafutaji. (Bw. Komba- Dar).

….Dada pole na majukumu. Napenda kumpa pole jamaa yangu aliyefanywa na mkewe kuwa hausigeli. Cha kumshauri kwanza, aachane kabisa na mwanamke huyo kwani anaweza hata kuhatarisha maisha yake.

Kuhusu mtoto apige moyo konde kwani mtoto akiwa mkubwa atahitaji kumwona baba yake na hapo ndipo atakapomtafuta maana huyo mkewe na mama mkwe wako wamemkalia vibaya.

Fikiria hadi wamempeleka gerezani hata kumuua wanaweza. Ni mimi Genya Richard toka Kiloxa(namba na majina vitoke) Simu:0682207565.
….Mwingine anasema; Aachane naye, huyo mtoto atakuja akikua, asiumize kichwa akazane na kazi. 0652887372 .

…Hujambo Flora. Mke kuwa mcharuko inatokana na aina ya mwanaume kuwa na mapungufu. Mwanamke akijaribu hivi mwanaume anaelekea kama mti unavyosukumwa na upepo. Piga uwa mwanaume sawasawa hawezi kuhamia kwa mwanamke. Huyo baba namshauri aende tamwa au mashirika ya kujitolea watamsaidia (temu).

…Pole sana. Avumilie afanye kazi mtoto atakuja siku moja(Jafar wa Arusha.)
Mpenzi msomaji, bila shaka umesikia maoni na ushauri wa wenzetu hao juu ya kijana anayepelekeshwa na mama mtoto wake.

Majanga ya aina hii yapo katika familia nyingi ila tu wengine wameziba midomo pengine wakichukulia ni ya kawaida au wanaona aibu kuyaweka hadharani.

Lakini mimi niwaambie. Hilo ni janga kama ambavyo linamtaabisha mwenzetu huyu. Angalia alikuwa na kazi amasitisha kwa kulazimishwa kulea. Tangu lini baba akaachwa nyumbani akalea watoto na mama akabeba mkoba akaenda kazini? Labda kama ana tatizo la afya au amefukuzwa kazini.

Lakini kama ana nguvu zake, akili timamu, kwanini baba akae nyumbani? Hilo ni jukumu la mama ambaye naye katika ulimwengu wa sasa anashukilia majukumu yote mawili (kutunza familia- malezi na kujishughulisha na kazi zingine za kuingiza kipato). Tabia hii ikomeshwe, tusiwageuzie kibao wanaume eti wakae nyumbani halafu kinamama waende kazini. HAPANA.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment