Tuesday, 18 August 2015

Hadithi yakusisimua:HUKUMU BILA KOSA

Nilirudi nyumbani nikiwa mchovu sana,mawazo kibao yamenitawala kichwani. Nilijiuliza mara kwa mara ni wapi mke wangu alipokwenda sikupata jibu lolote. Nilipiga simu kwa mashoga zake wote kuwauliza endapo mke wangu kipenzi Janeth yupo kwao. Jibu walilonipa lilinikata maini, nilishindwa kuelewa kilichomsibu mke wangu mpaka sasa haonekani nyumbani kwa siku tatu.
Nilishindwa kuyazuia machozi yaliyoteremka kufuata vifereji vya mashavu yangu mpaka mdomoni.Taarifa za kupotea kwa mke wangu Janeth sikupeleka polisi kwanza. Nilitaka nifanye uchunguzi mimi mwenyewe ili nijue mahali alipo.
Janeth kipenzi changu cha moyo. Yeye ndiye kila kitu kwangu, bila uwepo wake maisha yangu huwa mashakani. Nilikuwa napata homa endapo mke wangu atachelewe kutoka kazini hata kwa sekunde kumi tu. Si Mimi tu ambaye nilijawa na wivu juu yake hata yeye mwenyewe hakupenda nipotee kwenye uwepo wa macho yake hata saa moja.
Kama ingewezekana tungefanya kazi ofisi moja lakini ilishindikana kutokana na kusomea kazi tofauti. Yeye alikuwa mwandishi wa habari katika gazeti la “Msema kweli” lililokuwa linatoka Jumanne na Ijumaa. Mimi nilikuwa naendesha biashara zangu binafsi. Nina kiwanda cha kusindika maziwa na kusambaza nchi nzima na nchi jirani za Afrika Mashariki.
Mungu alitujalia tukawa na maisha mazuri,tulikuwa na nyumba mbili za kuishi maeneo ya Kimara Baruti. Vilevile nilifanikiwa kumjengea Mama yangu Nyumba ya Kisasa Kimara Bucha. Gari za kutembelea tena “New Modern” hazikutupiga chenga. Ni mwaka mmoja tu umepita toka tufunge ndoa mimi na Janeth.
Siku zote tulikuwa wenye furaha tele mpaka tukasahau kifo. Mwishoni mwa wiki tulipenda kutembelea kwenye kumbi mbalimbali za starehe kubadilisha mazingira. Siku moja moja tuliwatembelea wazazi kuwasalimia.
Siku moja furaha yangu ilipotea niliporudi nyumbani toka kazini. Siku hiyo nilichelewa kidogo tofauti na siku nyingine. Ilikuwa saa mbili usiku nilipopaki gari langu na kuingia ndani. Siyo kawaida ya Janeth kutokuwepo nyumbani muda huo labda kutokee dharura..
Nilishangaa sana kwa kuwa ni kitu ambacho hakikuwahi kutokea. Nilimtafuta kila chumba bila mafanikio, Nilipompigia simu hakupatikana kitu ambacho kilinitia wasiwasi zaidi. Nilitoka nje na kumuuliza mlinzi “ Rashidi; Janeth alipoondoka amekuaga .?”
“Hapana yeye alichukua gari hapa majira ya saa nane mchana na kuondoka zake, mpaka sasa hivi hajarudi”
“Kwani leo hajaenda kazini?”
“Kazini alikwenda lakini aliwahi kurudi”
“Okey sawa”Nilirudi ndani na kuingia moja kwa moja bafuni kisha nikaoga. Baada ya kuvaa niliamua kuandaa chakula mimi mwenyewe. Nilikiweka mezani na kuendelea kumsubiria mke wangu.
Mpaka saa sita usiku Janeth hakutokea. Moyoni niliumia mno. Simu yake haikupatikana mpaka muda huo. Nilitamani kupiga simu nyumbani kwao kumuulizia lakini niliona nitawasumbua Wazazi wake kwa kuwa ilikuwa usiku sana.
Hata kula sikula kitendo cha kutoweka kwa Janeth kilinifanya nishebe. Nilijitupa kitandani kujaribu kutafuta usingizi. Nilijigeuza huku na kule kitanda kizima,nilihisi baridi kali kwenye mwili wangu. Nilishamzoea Janeth alikuwa akinisitiri baridi kwa kumbatio lake.
Alinibembeleza kama mtoto mchanga.Bila kujijua nilijikuta nikipotelea usingizi mpaka asubuhi, Yote haya hunifanyia mara baada ya kunipa haki yangu ya ndoa inayoniacha hoi kitandani.
Leo yuko wapi? Nipo peke yangu nimejikunyata. Shuka zima limelowana kwa machozi nikimlilia mtu nisiyejua alikokwenda. “Iwapo Janeth hatoonekana tena nitawaeleza nini Wazazi wake wakanielewa,mwanzoni walinikataa lakini kwa msimamo wa Janeth iliwalazimu kunioza kwa shingo upande. Sasa wakijua mwanao kapotea mimi nitawajibu nini?”
Kichwa changu kiligonga kama nyundo. Mawazo tele yalinitawala, nisijue la kufanya. Mpaka pamekucha sijapata hata lepe la usingizi
Siku nzima nilifanya kazi ya kumtafuta Janeth kila kona,sikumpita shoga wake hata mmoja.Wote niliwatembelea kumuulizia mke wangu.
Hata wao wenyewe walishangaa kwa jinsi walivyomjua Janeth hakuwa na tabia kama hiyo,wengine wakanipa moyo “ Usijali Japhet mkeo atarudi tu, pengine kapata matatizo huwezi kujua” Walinipoza kidogo moyo lakini baada ya kuachana nao mawazo yalirudi upya.
“Janeth kwanini unanifanyia hivi mama? Umekumbwa na maswahibu gani mpenzi wangu?Mbona simu yako haipatikani? Naumia Janeth, naumiaaa! Nielekeze mahali ulipo moyo wangu wangu utulie”
Nilizungumza mwenyewe nikiwa ndani ya gari yangu kama kichaa. Nilirudi nyumbani hoi- binii-taaban. Tangu asubuhi sikupitisha kitu chochote kinywani mwangu tofauti na maji ya kunywa.Nilihisi njaa lakini kwa jinsi nilivyokuwa nimechoka nilimwagiza Rashidi nje akaninunulie chipsi angalau nijipoze.
Nilikuwa mnywaji wa pombe lakini si mlevi,hivyo baada ya kula zile chipsi nilizoletewa na mlinzi wa nyumba yangu bwana Rashidi nilifungua friji na kutoa chupa mbili za Wine. Nilimimina kwenye glasi na kuanza kunywa taratibu.
Siku hiyo nilizipania pombe nikiamini kuwa ndizo zitakuwa mbadala wa Janeth wangu.Glasi moja iliyojaa Wine niligugumia mdomoni kwa mara moja bila kujali uchungu wa pombe hiyo. Sikuwahi kunywa pombe nikalewa lakini siku hiyo ilikuwa “ too much”.
Mpaka usiku wa manane nilishamaliza chupa mbili za Wine na bia chupa tatu. Nilishindwa kujielewa, nguvu ziliniisha.Nilipojaribu kunyanyua mguu ili niliekee chumbani kulala nikashindwa . Nilihisi mguu wangu ni mzito kama mfuko wa simenti. Nililala palepale kwenye sakafu mpaka asubuhi.
Nilipoamka nilienda kujimwagia maji ili kuuweka mwili sawa. Sikuamini nilichokifanya kumbe nimekunywa pombe nyingi kiasi kile?Nilifanya usafi wa ndani haraka haraka.Baada ya kumaliza niliwasha gari yangu mpaka ofisini. Nilikuta kazi kibao zikinisubiri na ukizingatia siku iliyopita sikwenda kazini. Hofu juu ya mke wangu iliendelea kunitawala.
Sikufanya kazi kama ipasavyo kwa kuwa nilijawa na msongo wa mawazo nikimuwaza mke wangu. Nilirudi nyumbani jioni bila matumaini yoyote. Bado nilikuwa katika vita kali ya kifikra,nafsi ilinisuta, ilitaka niwataarifu wazazi wa Janeth lakini moyo ulipinga.
****************
chanzo:MTUNZI-FREDY MZIRAY

No comments:

Post a Comment