KLABU ya Yanga, jana ilitoa pole ya shilingi mil 1 kwa familia ya msanii maarufu wa filamu nchini, Steven Charles Kanumba, aliyefariki usiku wa kuamkia Jumamosi.
Kiasi hicho kilikabidhiwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Ghana, Keneth Asamoah aliyeambatana na Mghana mwenzake, Yaw Berko na viongozi kadhaa wa klabu hiyo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi fedha hizo nyumbani kwa marehemu, Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Mwesigwa Selestine, alisema msiba wa Kanumba, ni pigo kubwa kwa tasnia ya filamu nchini.
“Sisi Yanga tumesikitishwa sana na msiba huu kutokana na ukaribu ambao tulikuwa nao na msanii huyu pamoja na kazi zake nyingi ambazo tulikuwa tunazitazama na zilikuwa zinajenga na kuelimisha jamii ndo maana msiba huu umetugusa sana,” alisema Mwesigwa.
Aidha, Mwesigwa alisema kiasi hicho kidogo cha fedha, ni ishara ya kuguswa kwao na msiba huo uliowashtua wengi.
Mbali ya Mwesigwa, wengine waliokuwemo kwenye msafara huo, ni Salum Rupia na Ally Mayai ambao ni wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, pamoja na Ofisa Habari, Louis Sendeu.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa klabu hiyo Lloyd Nchunga, Rupia alisema amemuwakilisha Mwenyekiti wake ambaye alitarajiwa kufika baadaye.
Kwa upande wake Asamoah, alisema aliposikia kwa mara ya kwanza msiba wa msanii huyo, hakuamini kwa jinsi alivyowahi kumwona siku ya sherehe za kupongezwa kwa ubingwa wa Kombe la Kagame zilizofanyika katika ukumbi wa Nyumbai Lounge.
“Kifo cha Kanumba kinaniuma sana, maana huko nyuma nilikuwa nikimuona tu katika filamu mbalimbali, lakini nikaja kumuona siku ya sherehe za Kombe la Kagame, Mungu amlaze mahali pema peponi,” alisema Asamoah huku chozi likimtoka.
Katika hatua nyingine, Chid Mchome ambaye ni mwanakamati wa kamati mazishi alisema, marehemu Kanumba atazikwa keshoJumanne makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Alisema, kabla ya mazishi, mwili wake utaanza kuagwa majira ya saa 4:00 asubuhi.
“Tumepanga kuanza kuuaga mwili kuanzia saa 4:00 asubuhi kutokana na watu kutarajiwa kuwa zaidi ya elfu 20,” alisema Mchome.
No comments:
Post a Comment