Monday, 24 September 2012

MASHAUZI CLASSIC WAPATA AJALI DAR!!


GARI la kundi la mipasho la Mashauzi Classic Modern Taarab, alfajiri ya juzi, lilipata ajali baada ya kuzimika ghafla katikati ya barabara na kurudi nyuma kwa kasi na kuingia kwenye mtaro kando ya barabara.
Tukio hilo lilitokea maeneo ya Mtoni Kijichi, wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam, wakati gari hilo likiwarejesha nyumbani wasanii wa kundi hilo chini ya Mkurugenzi Mkuu, Isha Mashauzi ‘Jike la Simba’.
Meneja wa Mashauzi Classic, Suma Laga alisema jana kuwa, walikuwa wakitokea Tabata kwenye ukumbi wa Da’ West walipokuwa wakitumbuiza siku hiyo, wakielekea Mtoni Kijichi kumrudisha mpiga gitaa la besi, Amad Mominu.
“Wakati tunapandisha kilima cha kuiacha Mbagala Mission kuingia Kijichi, tukiwa tunakaribia kileleni, gari lilizimika ghafla na kuanza kurudi nyuma kwa kasi, wakati huo dereva akijitahidi kubana breki ambazo nazo zilikataa,” alisema Suma.
Suma alisema kuwa, baada ya jitihada za dereva kushindwa, gari hilo lilikwenda moja kwa moja na kugonga mtaro pembeni mwa barabara na wasanii kadhaa wameumia.
Aidha, alisema wasanii wanne wa kundi hilo, Zubeda Maliki, Asia Thabit (waimbaji), Ibrahim Kamongo (kinanda) na Goodluck Katambwa (mnenguaji), walijeruhiwa na kupelekwa hospitalini Mwananyamala ambako walitibiwa na kuruhusiwa.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment