Wednesday, 30 January 2013

Lulu arejea uraiani



HATIMAYE msanii wa filamu nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’, jana alipata dhamana baada ya kutimiza masharti matano aliyopewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, juzi.
Lulu anakabiliwa na kesi ya kumuua bila kukusudia aliyekuwa msainii mwenzake Steven Kanumba.
Lulu alitimiza masharti hayo jana saa 9 alasiri kwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Francis Kabwe.
Baada ya kutimiza masharti hayo ya dhamana, aliwaeleza waandishi wa habari huku akitokwa machozi kuwa anamshukuru Mungu, kwani yeye ndiye alifanya akapata dhamana hiyo na hivyo kumfanya atoke gerezani na kurejea kuishi uraiani.
Lulu ambaye alikuwa ameongozana na wakili wake Peter Kibatara, alisema anawashukuru wale wote waliokuwa naye bega kwa bega, tangu kesi yake ilipoanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
“Ninachoweza kusema ni kuwashukuru wale wote waliokuwa wakinihangaikia na kuniombea kwa Mungu hadi leo nimepata dhamana, narudi kuungana na familia yangu…lakini naomba watu hao waendelee kuniombea, kwani leo nimepata dhamana tu na ile kesi yangu ya msingi ya kuua bila kukusudia bado haijaanza kusikilizwa na kutolewa uamuzi, hivyo naombeni sana waendelee kuniombea na wasinitupe,” alisema Lulu.
Msanii huyo amedhaminiwa na Florian Matungwa, ambaye anatoka Wizara ya Ardhi na Verus Mboneko Wizara ya Afya.

Lulu alifikishwa eneo la Mahakama Kuu saa 7:58 mchana na gari ya Jeshi la Magereza lenye namba za usajili STK 2823. Baada ya kupatiwa dhamana, aliondoka na gari aina ya Land Cruiser VX V8, lenye namba za usajili T480 CFX.
Hata hivyo, Wakili Kibatara, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa kwa niaba ya mteja wake, anakanusha uvumi uliokuwa umeenea kuwa Lulu angeliachiwa kwa dhamana jana angeenda moja kwa moja kwenye kaburi alilozikwa Kanumba lililoko eneo la Kinondoni na kuongeza kwa kumshukuru Msajili Kabwe, kwa kumpatia dhamana mteja wake, kwani muda wa kazi ulikuwa umepita.
Mawakili wa Lulu, Peter Kibatara, Kennedy Fungamtama na Fulgence Massawe waliiomba mahakama hiyo impatie dhamana mshtakiwa huyo ambaye amesota rumande katika gereza la Segerea tangu Aprili mwaka jana, ambapo walieleza kuwa ombi la dhamana wameliwasilisha chini ya kifungu cha 148(1), (2) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 2002 .
Jaji Mruke alisema ili mahakama impatie dhamana ni lazima asalimishe kwa Msajili wa Mahakama hiyo hati ya kusafiria, kutotoka nje ya Dar es Salaam bila ruhusa ya mahakama, kuripoti kwa msajili kila mwezi, kuwa na wadhamini wawili ambao ni watumishi wa serikali ambao watasaini bondi ya sh milioni 20 kila mmoja.
Baada ya jaji huyo kutangaza masharti hayo, Lulu alishindwa kupata dhamana hiyo baada ya Msajili wa Mahakama kutokuwepo ofisini hiyo juzi.
Wasanii waliokuwepo kumuunga mkono Lulu mbali na mama yake mzazi mahakamani hapo, ni Mahsein Awadh maarufu Dk. Cheni, Muna na msanii mwingine ambaye jina lake halikupatikana mara moja.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment