Friday 11 October 2013

Wawili wafa maji Dar

WATU wawili wameripotiwa kufa maji katika matukio tofauti yaliyotokea juzi jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelibert Kiondo, alisema jana kuwa Kombo Shahame (22) mkazi wa Pemba, aliyekuwa akivua samaki, alikufa baada ya kuzama baharini alipokuwa akienda kurekebisha nyavu.
Alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 3:00 asubuhi katika Bahari ya Hindi, eneo la Sinda – Mji Mwema.
Kamanda Kiondo alisema kuwa wakiwa wanavua samaki kwa kutumia boti, kijana huyo alizama baharini kwa ajili ya kwenda kurekebisha nyavu, lakini alikaa muda mrefu bila kuibuka, jambolililowatia hofu wenzake ambao waliamua kujitosa kumfuata.
Alisema wenzake walifanikiwa kumpata akiwa amekunywa maji mengi huku akitokwa mapovu mdomoni na puani na akipumua kwa shida.
Kiondo alisema wavuvi wenzake walimuweka ndani ya boti ili kumuwahisha hospitali, lakini akiwa njiani alifariki dunia. Maiti imehifadhiwa Hospitali ya Vijibweni.
Katika tukio jingine, Elizabeth Simon (18), mkazi wa Majohe Kivule, amefariki dunia baada ya kutumbukia kwenye karo la maji machafu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alisema tukio hilo limetokea juzi, saa 10:00 jioni maeneo ya Majohe Kivule.
Minangi alisema akiwa maeneo hayo ghafla alitumbukia kwenye karo la maji machafu; aliokolewa na wananchi akiwa amekwisha kunywa maji mengi na kufariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Amana.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment