Wednesday 15 January 2014

Balozi wa China aibiwa simu Ikulu Zanzibar!!!

SHEREHE za maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar, zimekuwa chungu kwa balozi mmoja nchini, baada ya kuibiwa simu yake ya mkononi yenye thamani ya zaidi ya sh milioni moja.
Habari ambazo Tanzania Daima imezipata zilisema kuwa simu hiyo iliibwa katika mazingira ya kutatanisha wakati wa dhifa ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Ikulu ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya dhifa hiyo iliyohudhuriwa na watu maalumu, akiwemo Rais Jakaya Kikwete, balozi huyo alijikuta ameibiwa simu hiyo aliyokuwa ameweka kando ya meza aliyoketi na maofisa wa Ikulu  na wageni wengine waalikwa.
Hadi sasa haijulikani nani aliondoka na simu hiyo, lakini habari zaidi kutoka kwenye dhifa hiyo zinasema kuwa huenda simu hiyo ilichukuliwa na watu wa Idara ya Usalama kwa ajili ya mambo ya usalama.

Mmoja wa maofisa wa Ikulu ya Zanzibar ambaye aliomba jina lake lisitajwe, alikiri kuwa balozi huyo aliibiwa simu yake na hadi anaondoka kwenye dhifa hiyo hakuweza kuipata.
“Ni tukio la aibu sana, lakini kuna uwezekano mkubwa kwamba simu hiyo imechukuliwa kwa sababu za kiusalama,” alisema mtoa habari wetu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadamu Khamis Mkadamu, alisema kuwa hana taarifa za tukio hilo.
Alisema yeye alikuwa mtu wa mwisho kutoka kwenye hafla hiyo, hivyo hakukuwa na tukio hilo.
Alipobanwa zaidi, kamanda huyo alisema kama tukio hilo lipo, kuna uwezekano mkubwa wa simu hiyo kudondoka kwa bahati mbaya, lakini haiwezekani na si sahihi kusema imeibwa.
“Ile ilikuwa hafla maalumu, kwa watu maalumu, na walioalikwa ni watu wenye hadhi na heshima zao katika taifa hili. Hakuna mtu wa mtaani aliyeingia. Katika kundi lile sioni mtu wa kuiba simu, wote ni watu wazima, wenye heshima na nyadhifa kubwa ndani na nje ya nchi.
“Mimi mwenyewe juzi niliangusha kadi yangu, niliitafuta sana lakini siku moja dereva wangu wakati anafanya usafi wa gari aliiona. Kwa hiyo simu hiyo haiwezi kuibwa, ila anaweza kuwa ameidondosha au ameiweka sehemu ambayo hakuweza kuiona kwa wakati ule,” alisema kamanda huyo.
chanzo: tz daima

No comments:

Post a Comment