CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimesema migogoro ya ardhi inayoendelea sehemu mbalimbali nchini isipopatiwa ufumbuzi wa haraka itahatarisha amani na kufanya nchi isitawalike.
Pia chama hicho kimemwandikia Rais Jakaya Kikwete barua ya kumwelezea manyanyaso na mateso wanayopata wananchi wanaoishi katika bonde la Kiru, lililopo Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara kutokana na umilikishwaji wa ardhi kwa wawekezaji kinyume cha sheria.
Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia, alisema kwa kiasi kikubwa hali hiyo inasababishwa na wanasiasa kudharau wajibu wa wataalamu na kuingiza siasa katika kila jambo.
Alisema kutokana na hali hiyo ipo siku historia ya nchi itakuja kuwahukumu watu kwa matendo yao mabaya yenye dhamira ya kuliangamiza taifa kwa kigezo cha kulinda amani isiyokuwepo.
“Watanzania tuna mawazo mgando, leo hii hatufikiri vizuri, kwani tunashuhudia mambo ya kitaalamu yakifanywa kisiasa, hatuheshimu wataalamu kwa kufikiri sisi wanasiasa tuna mawazo kuwazidi wataalamu wetu hii si haki hata kidogo,” alisema Mbatia.
Alisema Tanzania hivi sasa ina vita kubwa ya maneno kutoka kwa watu wanaodhulumiwa haki zao, hali inayosababisha muda mwingi kutumika kufuatilia haki hizo na kuacha kufanya kazi itakayoweza kuboresha maisha ya wananchi hao.
Alisema ukiukwaji wa haki za binadamu katika bonde la Kiru ni mkubwa tofauti na watu wanavyofikiria, kwani maisha ya wakazi hao na wawekezaji waliopo katika maeneo hayo yamekuwa ni ya kuviziana kutokana na uhasama unaosababishwa na migogoro ya ardhi.
Alisema wakazi wa maeneo hayo wako katika simanzi nzito ya kutokujua nani atawasaidia na kumuomba Rais Kikwete kutumia mamlaka yake kuunda tume itakayoshughulikia suala hilo na kutoa maamuzi ya haki kwa anayestahili.
No comments:
Post a Comment