WATU wawili wameripotiwa kufariki dunia katika matukio tofauti yaliyotokea jijini Dar es Salaam, likiwamo la mtoto kutumbukia katika shimo la maji machafu.
Akielezea matukio hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile, alisema mtoto, Said Karim (6), mkazi wa Tabata –Mawenzi, alifariki dunia juzi, baada ya kutumbukia kwenye shimo la maji machafu.
Alisema mtoto huyo alitumwa kwenda dukani na kwa bahati mbaya alitumbukia katika shimo hilo. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Amana.
Katika tukio jingine, mwendesha pikipiki, Idi Kibwana (29) mkazi wa Tabata Kimanga amefariki dunia baada ya kugongwa na gari.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa nane mchana katika barabara ya New Bagamoyo.
Alisema gari T 794 BEG Coaster lililokuwa likiendeshwa na Adolph Kauma (31) liligonga pikipiki ambayo haikufahamika namba zake na kusababisha kifo cha dereva huyo.
Dereva aliyesababisha ajali hiyo anashikiliwa na polisi, mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala.
No comments:
Post a Comment