Saturday 16 July 2011

BWANA MISOSI KUWASHA MOTO NDANI YA BILICANAS!!!!!!!!!!!!




UKUMBI wa kimataifa wa Club Bilicanas, Jumapili unatarajiwa kupambwa na burudani ya kukata na shoka kutoka kwa msanii mahiri wa muziki wa bongo fleva, Joseph Rushahu maarufu kama Bwana Misosi.
Mkali huyo ambaye amekuwa akiibuka na kutoweka katika tasnia hiyo, atatumbuiza ukumbini hapo kupitia usiku maalumu wa Bongo Starz Nite ambao kwa Jumapili ijayo umebatizwa jina la ‘Usiku wa Misosi na Bwana Misosi’.
Bwana misosi ni mmoja kati ya wasanii waliojipatia umaarufu mkubwa hapa nchini na nchi jirani, hiyo inatokana na umahiri mkubwa katika utayarishaji wa kazi zake ambazo zimekuwa zikiwashika mashabiki.
Tayari Bwana Misosi amefanikiwa kuachia albamu tatu mpaka sasa, ambazo ni ‘Nitoke Vipi’ (2004),  ‘Kazi  Yangu’ (2006)  na ‘Pilato na Game’ (2011), huku singo ya ‘Kipusa’ aliyomshirikisha Prof. Jay ndiyo ilikuwa ya kwanza kwake, ambayo kwa kiasi chake iliweza kumtambulisha.
Singo ya ‘Nitoke Vipi’, ndiyo iliyomtambulisha katika medani ya muziki huo alipoanza rasmi mwaka 2005 ambapo ndani yake anawauliza mashabiki atoke vipi katika muziki huo. Kwa kifupi wimbo huo ulifanikiwa kukamata sana kuanzia kwenye redio, televisheni na hata kumbi za starehe.
Hakuishia hapo, kwani alikuja na singo ya ‘Mabinti wa Kitanga’ ambayo ndani yake ilikuwa ikielezea sifa za mabinti wa mkoani Tanga, ikiwamo kujua kujipamba, mapozi na mambo mengine.
Ukali wake unatokana na kuimba nyimbo zenye ujumbe mahususi kwa jamii, hivyo kumtofautisha na wasanii wengine; mfano katika singo ya ‘Pilato na Game’ aliomshirikisha Fid Q anazungumzia matatizo yanayoikumba sanaa ya muziki na wasanii kwa ujumla.
Pia mustakabali mzima wa muziki akizungumzia kuhusu wingi wa watayarishaji wa muziki kila mahali tofauti na zamani, huku akilinganisha mambo yanayotokea sasa katika muziki ni sawa na kilio ambacho anakileta kwa mashabiki ili wajue hasa nini kinachosumbua.
Katika moja ya mashairi yake kwenye wimbo huo Misosi anaimba: “…Maprodyuza kibao, sina imani na mwongozaji wa mchezo mpaka fulani ndo promo usogezwe, …refa anashabikia timu pinzani offside center hivi kweli nitawini….namuamini Mungu namba moja kitu gani, …nimejipanga simjui rafiki, adui, kasuku, kinyonga, simba, swala, mbogo na chui, si ufisadi sanaa ingekuwa mbali nafasi nikipewa nachekea nyavu kweli… ”.
Anaendelea: “Kwa mfano enzi za kifalme pilato watoza ushuru South Afrika enzi zile za Mkaburu, Tanganyika na mapinduzi ya uhuru, same time kumuweka wangu …wala sikufuru makamisaa wapo, refa anawaburuza, muuaji wa vipaji tapeli wanamtukuza, mashabiki nanyi mmelishwa limbwata kukubali tembo mtamu kuliko nyama ya bata, upande wao ni furaha….iwe ni mamba au kenge wanaongoza tu msafara….imani matendo ni tofauti na kuokoka…”.
Pia amewahi kutoka na singo kama; ‘Heshima’ aliyomshirikisha Red Sun kutoka Kenya, ‘Huwezi jua’ aliyomshirikisha Jua Cali kutoka Kenya, ‘Mungu yuko bize’ aliomshirikisha Chegge, ‘Nimesomeka’ aliomshirikisha Nikki Mbishi na nyingine kibao ambazo zote zimekuwa zikifanya vema.
Akiwa mmoja wa wasanii wenye asili ya Mkoa wa Kigoma, aliyekulia mjini Tanga ambao wanawakilisha vema katika medani ya muziki, Misosi amekuwa akija na kupotea katika tasnia hiyo, huku mwenyewe akidai kuwa ni kutokana na kutingwa na shughuli za ujenzi wa taifa, ikiwemo masomo.
 “Ukimya wangu ulikuwa unamaanisha, kwani nilikuwa darasani kwa ajili ya kujiendeleza kielimu, sasa hivi nimerejea rasmi kwenye game,” alisema Misosi ambaye alikuwa akisomea masuala ya teknolojia ya habari (IT).
Anaongeza kuwa, kwa sasa amerudi kwa nguvu zote huku akiwaomba mashabiki wa muziki huo nchini kuendelea kumuunga mkono katika kazi zake kama walivyokuwa wakifanya tangu aibuke.
“Mambo mazuri zaidi na zaidi yanakuja, mashabiki watarajie kazi nzuri kutoka kwangu, pia watarajie kuniona kwenye majukwaa ya muziki katika sehemu tofauti nchini na hata nje ikiwezekana,” alisema.
Mkali huyo ameweza kuwa mmoja kati ya wasanii bora wa muziki huo kiasi cha kushinda tuzo za muziki za Kili mwaka 2009/2010 kama mwimbaji bora wa reggae kupitia singo yake ya ‘Mungu yupo bize’.
Akizungumzia hali ya muziki nchini, Bwana Misosi anasema imekuwa ikikua kila kukicha, na hivyo kuwepo kwa ushindani mkubwa baina ya wasanii na wasanii na bila kuumiza kichwa msanii anaweza kujikuta akibaki kuwa msindikizaji kama si kushindwa kufanya alichokusudia.
Hata hivyo, Bwana Misosi anasema ni wasanii wachache ambao wameweza kudumu katika medani hiyo hiyo kwa muda mrefu, na hiyo inatokana na umakini walionao na kutambua nini wanachokifanya.
 “Wengine wanaingia kwa kufuata mkumbo, kupata umaarufu n.k, lakini mambo ya ulimbukeni, utovu wa nidhamu na kuvimba kichwa ni baadhi ya mambo yanayochangia kuwamaliza wasanii wengi katika muziki,” anasema
Akiwa na matarajio ya kufika mbali zaidi katika medani hiyo, mkali huyo pia anawaasa wasanii wenzake kujiheshimu sambamba na kutunga nyimbo zenye ujumbe muhimu kwa jamii badala ya kuimba sana nyimbo za mapenzi

No comments:

Post a Comment