MSANII wa filamu nchini, Kajala Masanja na mumewe Faraja Chamba, jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na makosa matatu likiwemo la kutakatisha fedha haramu.
Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKUKURU), Leonard Swai mbele ya Hakimu Mkazi Sundi Fimbo, alidai washtakiwa ambao wanatetewa na wakili wa kujitegemea, Alex Mgongolwa, wanakabiliwa na makosa matatu.
Wakili Swai alidai kuwa, kosa la kwanza ni la kula njama kinyume na kifungu cha 34 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007 ambapo washtakiwa wote kwa pamoja walitenda kosa hilo la kula njama la kuhamisha miliki ya nyumba iliyopo Kunduchi Salasala jijini Dar es Salaam.
Shitaka la pili, ni kwamba Aprili 14, 2010 walihamisha isivyo halali umiliki wa nyumba hiyo kinyume na kifungu cha 34(2)A(3) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.
Alidai shitaka la tatu ni la kutakatisha fedha ambalo walilitenda siku hiyo ya Aprili 14 mwaka 2010 huku wakijiua ni kinyume na sheria hiyo.
Hata hivyo, mshtakiwa wa pili (Chamba) wakati wanasomewa mashtaka hayo jana hakuwepo mahakamani kwa sababu yupo gerezani akikabiliwa na kesi nyingine ya utakatishaji fedha ambayo ipo katika mahakama hiyo na kwa mujibu wa sheria kosa la kutakatisha fedha halina dhamana.
Kajala alikanusha mashtaka hayo na wakili Swai alidai upelelezi bado haujakamilika.
Hakimu Fimbo aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 20, itakapokuja kwa ajili ya kutajwa na akaamuru Kajala arudishwe rumande kwa sababu kosa la kutakatisha fedha linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
No comments:
Post a Comment