OFISA elimu wa shule za msingi wa jiji la Mbeya Aurelia Lwenza amepewa angalizo na wazee wa kimila wa kata ya Iganzo iliyoko jijini hapa kutoingilia masuala ya imani za kishirikina wanazotuhumiwa walimu wake.
Wazee hao wametoa angalizo hilo wakitaka kutomuona mwalimu wa shule ya msingi Juhudi Mwalimu Eliud Kyando aliyefukuzwa shuleni hapo na wananchi wa kata hiyo baada ya kutuhumiwa kuwa mchawi.
Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule hiyo hapo machifu hao walisema kuwa baada ya kumbaini kuwa anajihusisha na mambo ya kishirikina shuleni hapo waliamua kumfukuza ili kunusuru maisha ya wanafunzi na walimu wao na kwamba alikuwa kikwazo cha maendeleo ya elimu shuleni kwa muda mrefu.
Walisema kuwa mwalimu huyo alikuwa akijihusisha na mambo hayo ya kishirikina ambapo mara kadhaa mwalimu mkuu wa shule hiyo Charles Mvella alikuwa akikuta vitu vya ajabu ofisini kwake vikiwemo vinyesi, kondom na vitabu kuzagaa hovyo vilivyokuwa vimepangwa kabatini huku mlango ukiwa umefungwa kama kawaida hali iliyompelekea kuwarudisha wanafunzi kuwaita wazazi ili wafike shuleni hapo kujulishwa hali ilivyokuwa ikijitokeza mara kwa mara.
Aidha walisema kuwa baada ya wazazi hao kufika shuleni hapo kumsikiliza mkuu huyo wa shule, walidai kuwa walielezwa hali halisi iliyopo shuleni hapo ndipo wazee wa kimila (machifu) wakaanza kutafiti anayehusika kwa njia za kimizimu hali iliyompelekea kubainika kwa mwalimu huyo kuwa ndiye anayefanya mambo hayo ya kishirikina.
Chifu Leonard Lunile alisema kuwa baada ya kumbaini mwalimu huyo ndiye anayefanya mambo hayo tulimuonya lakini hakutaka kusikia na kuacha tabia yake ya kishirikina ambapo wananchi wakaamua kwenda nyumbani kwake kumvamia na kumshambulia kwa kumpiga mawe hadi alipookolewa na jeshi la polisi waliofika eneo hilo mapema na kunusuru uhai wake.
“Sisi tulimuonya aache tabia hiyo hakusikia ndiyo maana wananchi wakapandwa na hasira na kumfuata nyumbani kwake na kuanza kumshambulia kwa kumpiga mawe hadi alipookolewa na polisi hata hivyo sisi machifu tunasema hivi asionekane tena jijini hapa akionekana tutajua cha kumfanya; walikuwepo wengi kama yeye na sasa hawapo hawezi kutushinda,” alisema chifu huyo.
Hata hivyo wananchi waliokuwa wamefurika shuleni hapo waliendelea kusema kuwa mwalimu huyo hakuwa peke yake mwenye tabia hiyo bali wapo walimu wengini wanaojihusisha na imani za kishirikina hatua iliyowapelekea diwani wa kata hiyo ya Iganzo Uswege Fullikah na ofisa elimu huyo Aurelia Lwenza kutoa nafasi kwa wananchi hao kuwataja walimu wanaohusiwa na ushirikina huo.
Ndipo wananchi hao wakaamua kupiga kura za siri ili kuwabaini walimu wanaojihusisha na mambo hayo ambapo ofisa elimu huyo akakubaliana na hoja hiyo na kuanza kupiga kura hizo na baada ya zoezi hilo kura hizo hazikuhesabiwa hapo hapo; aliondoka nazo ofisa huyo na kudai kuwa atarudisha matokeo ya kura hizo ambapo hukubainisha siku ya kurejesha.
Taarifa zaidi zinasema kuwa mwalimu huyo alikuwa akifanya hivyo kwa lengo la kutaka madaraka shuleni huku akisaidiwa na baadhi ya viongozi walioondolewa katika kamati ya shule hiyo baada ya uchaguzi mpya wa kamati ya shule; ndiyo maana kila alipokuwa akionywa na wazee hao hakutaka kusikia.
No comments:
Post a Comment