Thursday, 3 May 2012

RAILA:MUDAVADI HURU KUONDOKA ODM.


Akizungumza na BBC mjini London, Odinga amesema kama kiongozi anayetetea demokrasia, hawezi kushtumu uamuzi wa naibu wake ambaye amejiuzulu pia kama waziri wa serikali za mitaa.
Aidha Odinga ambaye ni kiongozi mkuu wa chama cha ODM amesema ataachia baraza kuu la chama kuamua ikiwa itamuondoa kwenye chama Mudavadi na hivyo kupoteza kiti chake cha ubunge hatua ambayo huenda ikamfanya Naibu Waziri Mkuu kurudi kwenye uchaguzi katika jimbo lake la Sabatia, Magharibi mwa Kenya.
Kuhusu ikiwa ODM itayumba kisiasa kufuatia kuondoka kwa Mudavadi, Odinga amesema chama hicho kina wafuasi wengi na kujiondoa kwa Mudavadi hakuna athari zozote.
Tofauti kati ya Musalia Mudavadi na Raila Odinga zilichochewa na kanuni za uteuzi wa mgombea wa Urais wa ODM ambapo wanaomuunga mkono Mudavadi ulilalamika kuwa washirika wa Waziri Mkuu walipenyeza vipengele vinavyomzuia Naibu Waziri Mkuu kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho.
ODM imekumbwa na mpasuko mkubwa miongoni mwa wanasiasa wake ambapo tayari aliyekua naibu kiongozi wa chama hicho William Ruto alikihama chama na kufuatwa na wabunge waliomuunga mkono.
Nchini Kenya wabunge wamekuwa wakihama hama vyama ambavyo viliwafadhili kuingia bungeni bila kuwasilisha waraka wa kuachia ubunge kama inavyotakiwa kisheria.
                      HABARI NA BBC SWAHILKI

No comments:

Post a Comment