MSANII wa filamu nchini Sadiki Juma Kilowoko (Sajuki) anasafirishwa kuelekea India kwa ajili ya matibabu baada ya kukamilika kwa asilimia kubwa ya michango iliyotolewa na wasanii na wadau mbalimbali wa tasnia ya filamu.
Akizungumza na gazeti hili, Rais wa Shirikisho la Wasanii Tanzania, Simon Mwakifamba alisema kuwa msanii huyo ataongozana na watu wengine wawili katika safari yake hiyo.
Akizungumzia hali ya msanii huyo, Mwakifamba alisema kuwa anaendelea vizuri na kusisitiza kuwa wamepata asilimia kubwa ya fedha iliyokuwa ikihitajika kwa ajili ya matibabu yake.
Alisema kuwa zaidi ya Sh milioni 25 zilikuwa zikihitajika kwa ajili ya kumtibu msanii huyo ambapo wamepata Sh milioni 16 pamoja na tiketi tatu za ndege.
Alisema kuwa fedha hizo zitasaidia kwa kuanzia na kuongeza kuwa michango mingine inazidi kuchangishwa na zitatumwa kwa ajili ya kuendelea na matibabu zaidi.
Mwakifamba mbali na kushukuru kwa misaada iliyopatikana, alibainisha kuwa ugonjwa wa Sajuki umewafumbua macho na kuwafanya kama shirikisho kuwa na mikakati mipya yakuwasaidia wasanii wanachama wa shirikisho hilo.
Alisema kuwa kwa sasa shirikisho hilo limeingia makubaliano na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuhakikisha kuwa wasanii wanajiunga na bima ya afya ambapo watakuwa wakichangia
Sh 20,000 kila mwezi.
Alisema kuwa katika kuchangia fedha hizo wasanii pamoja na ndugu zao watatu watakuwa wakitibiwa ambapo aliwasihi wasanii kujitokeza kwa wingi kujiunga na shirikisho hilo.
“Najua wasanii wengi wanaishi maisha ya ujana na kushindwa kuangalia hatima ya uzee wao itakuwaje,” alisema.
Alisema, shirikisho limekubaliana na NSSF katika kuhakikisha kuwa wasanii wanaingia makubaliano ya mikopo ya nyumba.
Sajuki anasumbuliwa na tatizo la uvimbe tumboni.
HABARI NA : http://www.habarileo.co.tz/michezo/?n=29854&cat=michezo
No comments:
Post a Comment