Sunday 8 July 2012

VIONGOZI WA DINI WAJITOSA SAKATA LA DR.ULIMBOKA



VIONGOZI wa dini za Kikristo na Kiislamu wamejitosa katika sakata la Dk Steven Ulimboka ambaye yuko nchini Afrika Kusini kwa matibabu baada ya kutekwa na kupigwa na watu wasiojulikana pamoja na mgomo wa madaktari kwa kufanya mkutano na viongozi wa Jumuiya ya madaktari na wanaharakati jijini Dar es Salaam jana.
Viongozi hao walipendekeza iundwe kamati huru ya kuchunguza tukio la kupigwa Dk Ulimboka mapema iwezekanavyo ili kupata ukweli wa kilichotokea.
Pia viongozi hao walishauri kuwa Rais Kikwete akutane na madaktari pamoja na viongozi wa dini ili kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wao unaoendelea nchini hivi sasa.Viongozi hao pia wameitaka Serikali kutoa ulinzi kwa Dk Ulimboka na madaktari wote wengine ili kuwahakikishia usalama wa maisha yao.
Akisoma tamko la viongozi hao, Mkurugenzi wa Baraza la Habari la Kiislamu(Bahakita), Hussein Msopa kwa niaba ya viongozi hao alisema kwamba, kuundwa kwa kamati huru ya uchunguzi  itasaidia kupata ukweli wa tukio la kutekwa na kupigwa kwa Dk Ulimboka na kuwezesha  kubaini wahusika wa tukio hilo.
“Tukio la kutekwa, kuteswa na kutupwa katika Msitu wa Pande Dk Ulimboka ni la kusikitisha… na tunamuomba Rais Kikwete aunde tume huru itakayojumuisha madaktari wenyewe, viongozi wa dini, wanaharakati na wanasheria kubaini kiini cha tatizo hilo.” alisema Msopa.
Kauli ya viongozi hao wa dini ni ya kwanza kutolewa kwa pamoja tangu kutokea kwa tukio la kutekwa, kupigwa na kutupwa kwa Dk Ulimboka katika Msitu wa Pande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Viongozi hao pamoja na kudai tume huru pia waliomba Serikali kufuta kesi  iliyofungua dhidi ya madaktari waliofukuzwa kutokana na mgomo na  kuwarejesha kazini ili  kumaliza mgomo huo waliodai unaathiri afya za Watanzania.
Tamko hilo limekuja siku chache tangu Serikali  ilipofungua kesi dhidi ya madaktari waliogoma kwa Baraza la Madaktari Tanzania ikilitaka kufanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki kwa madaktari hao.
Msopa alitaja sababu ya viongozi hao kuungana na wanaharakati kutafuta suluhisho la mgomo huo kuwa ni kuona Watanzania wanazidi kuteseka kwa kukosa huduma za matibabu.
“Tunafahamu kwamba, Rais Kikwete ameweza kutatua migogoro mingi mfano mgogoro wa Chadema, suala la Katiba Mpya, migogoro ya Zanzibar, hivyo pia sasa tunaamini katika hili la madaktari ataweza kulitafutia ufumbuzi,” alisema Msopa.

No comments:

Post a Comment