Juma Mtanda na Hamida Shariff, Morogoro
VURUGU kubwa zimezuka mjini Morogoro baina ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Polisi na kusababisha kifo cha mtu mmoja anayedaiwa kuwa mfuasi wa chama hicho cha upinzani.Tukio hilo lilisababisha taharuki kubwa katika eneo kubwa la Manispaa ya Morogoro, huku wanachama na baadhi ya viongozi wa chama hicho wakionekana kuzagaa katika maeneo mbalimbali yakiwamo ya mjini na Hospitali ya Mkoa alikopelekwa maiti huyo na polisi kwa lengo la kupata taarifa zaidi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shillogile alithibitisha kutokea kwa kifo hicho lakini akasema haijathibitishwa kwamba aliuawa kwa bomu, risasi au ajali na kwamba jeshi hilo linafanya uchunguzi kujua chanzo cha kifo chake.
Hata hivyo, alisema polisi walilazimika kutumia risasi za moto kuwatawanya wafuasi wa Chadema baada ya chama hicho kukaidi agizo lililowataka wasifanye maandamano.
Kifo hicho kilitokea katika eneo la Msamvu ambako wafuasi hao walikusanyika, wengine wakitokea Barabara ya Dar es Salaam na wale waliokuwa wakitokea Barabara ya Dodoma, tayari kuwapokea viongozi wa kitaifa wa Chadema.
Mfuasi huyo aliyefahamika kwa jina la Ally Zona (38), Mkazi wa Kihonda ni mpigadebe kwenye Kituo cha Mabasi Msamvu.
Taarifa za awali zilizolifikia gazeti hili, zilieleza kuwa Zona alifariki dunia wakati polisi wakirusha mabomu ya machozi na risasi kuwatawanya wafuasi wa chama hicho waliokuwa wakijiandaa kuandamana na baadaye kuhudhuria mkutano katika Uwanja vya Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege.
Tukio hilo lilitokea jana saa 7:30 mchana.
Ilivyokuwa
Baada ya wafuasi hao kukusanyika Msamvu tayari kuanza maandamano, polisi walitoa amri ya kuwataka watawanyike, lakini walikaidi hivyo kuamua kurusha mabomu ya machozi na risasi hewani kuwatawanya kitendo ambacho kiliwafanya wafuasi hao kutawanyika na kukimbia ovyo.
Kamanda Shillogile alisema baada ya tukio hilo na taarifa za kifo cha mfuasi huyo wa Chadema, ameamua kutuma askari kwenda katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mkoa ili kushirikiana na madaktari kuchunguza sababu za kifo hicho.
“Uchunguzi huo utabaini kama mtu huyo amefariki kutokana na bomu, risasi au ajali kwani wakati wa vurugu hizo watu walikuwa wakikimbia ovyo kwa kutumia magari na pikipiki,” alisema Shillogile na kuongeza:
“Kutoka eneo lililokuwa na vurugu hadi alipookotwa marehemu huyo, pana umbali kidogo kwa hiyo uchunguzi huo ndiyo utakaoeleza ukweli.”
Alisema kuwa uchunguzi wa awali, unaonyesha kwamba mwili wa Zona ulikutwa ukiwa unatoka damu kichwani kutokana na jeraha ambalo haijafahamika limetokana na nini.
Hata hivyo, Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu alidai kwamba kifo hicho kimetokana na risasi aliyopigwa kichwani na siyo bomu... “Kwa kitendo hicho polisi wanaonekana kuwa walifanya kusudi na walidhamiria kuua.”
Alisema mwili wa marehemu hautazikwa mpaka uchunguzi wa kidaktari utakapofanyika. Aliwataka walioshuhudia tukio hilo kujitokeza kutoa ushahidi ili askari waliohusika wachukuliwe hatua.
Alisema Chadema kimemteua Mwanasheria wake wa Mkoa wa Morogoro, Aman Mwaipaya kushuhudia wakati uchunguzi huo ukifanywa.
ENDELEA KUSOMA HAPA:http://www.mwananchi.co.tz/component/content/article/37-tanzania-top-news-story/25796-polisi-yawatawanya-chadema-kwa-mabomu.html
No comments:
Post a Comment