Mkazi wa kijiji cha Nyanze mkoani Simiyu, Mrisha Mshashi (70), anadaiwa kujitia kitanzi kupinga hukumu iliyompa ushindi mtalaka wake iliyotolewa hivi karibuni na mahakama ya mwanzo mkoani humo.
Katika hukumu hiyo Mahakama ya Mwanzo ya Mwandoyo mkoani Simuyu, ilitoa ushindi kwa mkewe (jina linahifadhiwa) kwa kumuamuru mwanaume huyu, kumlipa mkewe mashine ya kusaga nafaka, ng’ombe 10 na mabati 10 hukumu ambayo Mshashi hakuridhika nayo.
Kamanda wa Polisi Mkoa Simiyu, Salumu Msangi, alisema Mshashi alidaiwa kutumia kamba ya mkonge kumaliza maisha yake.
Aliongeza kuwa tukio hilo lilitokea Jumanne wiki hii baada ya Mahakama ya Mwanzo ya Mwandoya kutoa uamuzi huo.
Katika tukio jingine mwanakijiji mwingine alipoteza maisha baada ya kunywa kiasi kikubwa cha gongo.
Kamanda Msangi alimtaja marehemu kuwa ni Richard Lutoja (60) mkazi wa kijiji cha Igunja wilayani Maswa aliyefariki dunia Jumanne saa 1:00 jioni .
Kwa mujibu wa maelezo yake pombe hiyo ilikuwa ikiuzwa na Magogo Lufungula (56) pia mkazi wa kijijini humo. Kufuatia kifo hicho polisi inamshikilia Lufungula ambaye ni muuzaji wa gongo pamoja na Nonga John(50), aliyekuwa akinywa pombe na mteja huyo na kwamba washitakiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi wa polisi kukamilika.
Na katika tukio jingine Kamanda Msangi alisema jeshi hilo linamshikilia, Mwashana Sitta(44) mkazi wa kijiji cha Kiloleli wilayani Busega kwa kukutwa na lita 100 za gongo na kilo tano za bangi katika mkasa uliotokea Novemba 6 mwaka huu.
Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani wakati wowote
chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment