Saturday, 29 June 2013
Josephine Michael azalishwa naTrafiki barabarani.
BINTI mmoja aitwaye Josephine Michael mkazi wa Kijiji cha Kiegea nje kidogo ya Manispaa ya Morogoro, Jumatano iliyopita alijifungua barabarani wakati akikimbizwa hospitalini kwa kutumia usafiri wa bodaboda.
Tukio hilo lililowashtua watu wengi lilitokea asubuhi kwenye Kituo cha Daladala Cha Nanenane kandokando ya Barabara Kuu iendayo Dar es Salaam.
Askari wa kike wa kikosi cha usalama barabarani ‘trafiki’ (jina lake halikupatikana) akiacha kazi ya kuongoza magari na kugeuka mkunga kwa muda ili kumsaidia binti huyo akiwa sambamba na wanawake wengine na kufanikisha kupatikana kwa mtoto wa kiume ‘dume la nguvu’.
Awali, wanawake hao walizungusha kanga ili kuweza kuweka usiri wakati wa kumsaidia mwanamke mwenzao alipokuwa akijifungua.
Mara baada ya zoezi hilo kwenda salama, Josephine alisema alipatwa na uchungu alfajiri ya siku hiyo na mume wake aliwapigia simu madereva wa teksi zaidi ya wawili ambao waligoma kufika kijijini kwao kutokana na ubovu wa barabara.
“Hali ilipozidi kuwa mbaya tuliwasiliana na dereva wa bodaboda ambaye alifika na kunibeba huku mume wangu akitufuatilia nyuma kwa baiskeli yake,” alisema Josephine kwa uchangamfu.
Binti huyo alisema kwamba walipofika eneo la Nanenane hali ilizidi kuwa mbaya akashindwa kujizuia baada ya mtoto kushuka chini, hivyo akamuomba dereva wa bodaboda asimame ndipo alipoanguka chini na hali kuzidi kuwa mbaya.
Baada ya kuliona tukio hilo, trafiki na wanawake wengine waliokuwa jirani wakajitolea kumsaidia hadi alipojifungua salama.
Dereva wa bodaboda aliyembeba Josephine anayejulikana kwa jina la Gitogo Shilagi alikiri barabara iendayo Kijiji cha Kiegea kuwa mbovu.
chanzo:globalpublishers
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment