Saturday, 29 June 2013

Polisi jijini Mwanza linatuhumiwa kumuachia mtuhumiwa Jackson Robert maarufu kwa jina la Masamaki

JESHI la Polisi jijini Mwanza linatuhumiwa kumuachia mtuhumiwa aliyetajwa na watu waliokamatwa katika tukio la ujambazi, kuwa ndiye mfadhili mkuu wa matukio ya ujambazi jijini humo na maeneo mengine ya nchi.
Mtuhumiwa anayelalamikiwa kuachiwa kutokana na amri ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DCI), Robert Manumba, ametajwa kuwa Jackson Robert maarufu kwa jina la Masamaki ambaye aligombea udiwani katika Kata ya Kirumba kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Tanzania Daima, imepata taarifa kutoka jijini Mwanza kuwa Juni 23, mwaka huu watuhumiwa watatu ambao ni Anthony Joachim, Sylvester Saimon na mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Siri, walikamatwa katika eneo la Nyamanoro wakiwa katika harakati za kutaka kufanya uhalifu.
Inaelezwa kabla ya watuhumiwa hao kukamatwa, Sylvester aliwarushia askari risasi ingawa hakufanikiwa kuwajeruhi, na baada ya kudhibitiwa alimtaja Masamaki kuwa mfadhili wao aliyewapatia silaha waliyokutwa nayo.
Kutokana na maelezo hayo, polisi walifika nyumbani kwa Masamaki eneo la Igore Kirumba kufanya upekuzi uliofanikisha kukutwa kwa maboksi ya risasi yakiwa yamehifadhiwa.
Tanzania Daima limedokezwa kuwa baada ya upekuzi huo, polisi waliamua kuondoka na mtuhumiwa hadi kituoni ambako mahojiano zaidi yaliendelea.
Mtoa taarifa alilieleza Tanzania Daima kuwa wakiwa katika kituo cha polisi Kirumba lilifunguliwa faili lenye namba MZN/RB/4686/2013 kesi ikiwa ni unyang’anyi wa kutumia silaha. Kisha Masamaki aliomba kufanya mawasiliano na Christopher Gachuma, ambaye ni mjumbe wa NEC ya CCM taifa kupitia Mkoa wa Mara.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa baada ya muda watuhumiwa waliondolewa katika kituo hicho cha polisi na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi cha Centre.
“Pale kituoni siku ile walilala na Juni 24 Masamaki akaachiwa kwa dhamana. Nasikia Gachuma aliongea na DCI Manumba, wale wana undugu, na baada ya muda Ofisa Upelelezi wa Mkoa (RCO) akapigiwa simu ya kumuachia kwa dhamana. Lakini wenzake wanaendelea kushikiliwa,” alisema mtoa taarifa wetu jijini humo.
Aliongeza kuwa baada ya Masamaki kuachiwa faili liliandaliwa huku kukiwa na mkakati wa kumuondoa mtuhumiwa huyo katika sakata hilo, na kwamba baada ya faili kurejeshwa kutoka kwa DCI, jina lake halikuwepo kati ya watu wanaopaswa kupelekwa mahakamani.
Tanzania Daima iliwatafuta Gachuma, DCI Manumba na RPC wa Mwanza kwa ajili ya kupata ukweli wa kumuachia mtuhumiwa huyo.
Kauli ya Gachuma

Gachuma alipopigiwa simu kuulizwa juu ya kumkingia kifua Masamaki asijumuishwe na watuhumiwa wenzake wa unyang’anyi kwa kumuomba DCI Manumba aingilie kati, alikana kuhusika.
Alisema hadi leo hii hajui kama DCI Manumba amesharejea nchini kutoka Afrika Kusini alikopelekwa kwa ajili ya matibabu akitokea hospitali ya Agha Khan ya jijini Dar es Salaam.
“Mimi nipo Dodoma, huyo Manumba sina mazoea ya kuongea nae kwenye simu. Si nilisikia anaumwa, kwani amesharudi? Jamani hawa watu wanaonihusisha na mipango hiyo wana lao jambo,” alisema Gachuma.
DCI Manumba
Manumba alipopigiwa simu juu ya suala hilo, alisema hana taarifa hizo na kumtaka mwandishi azungumze na kamanda wa polisi jijini Mwanza lilikotokea tukio hilo.
Tanzania Daima ilipotaka kujua ilikuwaje akatoa maagizo kwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Mwanza ili wamuachie kada huyo wa CCM, hakujibu na akakata simu.
RPC Mwanza
Kamanda wa Polisi jijini Mwanza, RPC Ernest Mangu, alikiri jeshi hilo kumuachia Masamaki, lakini si kwa sababu ya maagizo ya DCI bali ushahidi uliopatikana.
Mangu alisema taarifa za polisi kumuachia Masamaki kwa shinikizo fulani zinalenga kuwachafua na zinatolewa na watu wenye nia ovu.
Alisema polisi walifanya uchunguzi na kubaini Masamaki hahusiki na watu waliokamatwa katika tukio hilo, na hata walipopeleka faili kwa mwendesha mashtaka wa serikali, akaona hakuna sababu ya kumfikisha mahakamani.
“Sisi ndio tunaopeleleza na kujiridhisha, sasa hao wanaosema tumepewa amri ya kumuachia watakuwa na sababu zao. Lakini ukweli ni huo, imeonekana hakuna sababu za kumfikisha mahakamani,” alisema Mangu.
Alipoulizwa sababu ya watuhumiwa kumtaja Masamaki ndio aliyewapa silaha pamoja na kukutwa kwa maboksi ya risasi nyumbani kwake, alisema silaha iliyotumiwa na watuhumiwa haikutoka kwa Masamaki na kwamba waliomtaja wanaweza kuwa na chuki naye.
chanzo: Tanzania daima

No comments:

Post a Comment