Thursday, 4 April 2013
Ridhiwan anakejeli utawala wa baba yake?
LEO sijatumwa mambo mengi, nimetumwa mambo mawili tu. La kwanza nimetumwa kuwakumbusha Watanzania tuwaombee ndugu zetu waliofariki katika ajali ya jengo la ghorofa, pale Mtaa wa Indira Gandhi jijini Dar es Salaam.
Mwenyezi Mungu awaangazie mwanga wa milele marehemu wapate rehema za Mungu, wapumzike kwa amani - Amina.
Tusisahau pia kuwaombea wanaohuzunika na msiba huo kwa kufiwa na ndugu, jamaa, marafiki zao na wategemezi wao ili Mungu awape ujasiri wakati huu wa msiba.
Tusiwasahau hata ndugu zetu wa Arusha, eneo la Moshono waliofunikwa na kifusi wakati wanapakia kokoto ili kujipatia riziki halali kwa kazi ya mikono yao, wote Mungu awarehemu.
La pili, nimetumwa na baadhi ya Watanzania tuangalie kauli ya Ridhiwan Jakaya Mrisho Kikwete, Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka Bagamoyo.
Kijana huyu amezungumza vitu vizito wiki hii. Akijibu swali kuhusu mwelekeo wa siasa nchini, amenukuliwa na gazeti moja la kila wiki nchini akisema: “Mwelekeo wa siasa una dalili mbaya, mauaji ya viongozi wa dini, mauaji ya wanaharakati, ukitafuta chanzo, chanzo ni kwa baadhi ya watu kufikia malengo yao.
“Mauaji kwa mfano ya padre Zanzibar, kuteswa Kibanda, Ulimboka au mauaji ya Chacha Wangwe hayakutokea kwa bahati mbaya. Inaonesha kuwa upo mkakati wa baadhi ya watu.”
Nimependa sana kauli ya kijana huyu kutoka Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani. Yawezekana amesema kwa bahati mbaya au amekusudia kusema, ila Watanzania wenzangu ndio wamenituma niulize maswali mazuri kwa Ridhiwan.
Je, alikuwa anakejeli utawala wa baba yake kuwa ameshindwa au amesema kwa bahati mbaya? Vyombo vya dola anavyotaka vichukue hatua, kiongozi wake si baba yake?
Kuhusu mauaji ya Chacha Wangwe, zilitengenezwa propaganda kuwa viongozi wa CHADEMA walihusika, baadaye wananchi waliona propaganda za CCM ni upuuzi, wakazipuuza, ndiyo maana baada ya kifo hicho walikipatia chama hicho ushindi mkubwa kupitia Charles Mwera.CCM pamoja na kwenda na helkopta mbili walikimbia kabla ya jogoo kuwika. Hii propaganda ilikufa, hatujajua inafufuliwa kwa sasa na kijana huyu kwa malengo yapi? Hapo ndiyo wazee wa Nyamisangura, Ronsoti na Bomani kule Tarime wameniomba nikuombe ufafanue vizuri, hujaeleweka.
Ridhiwan amezungumzia kuhusu kuteswa Dk. Ulimboka. Dk Ulimboka ndiye anayejua waliomtesa, anajua waliompigia simu hadi akatekwa.
Mamlaka ya Mawasiliano na polisi wanajua aliyetumia simu kumwita Dk. Ulimboka hadi alipoteswa.
Dk. Ulimboka mwenyewe amemtaja kuwa ni Ramadhani Ighondu, ambaye bila shaka Ridhiwan unakaa naye mara kadhaa Ikulu. Polisi hawajamwita kumhoji, wala mwenyekiti wa chama kinachoongoza serikali ambaye kwa mujibu wa maelezo yako umesema unamheshimu.
Muulize kwanini Ramadhani Ighondu hajakamatwa hata kuhojiwa kidogo wakati ametajwa na Dk. Ulimboka?
Vyombo vya dola ambavyo Ridhiwan anataka vichukue hatua, viliunda tume, havijawahi kukamata mtu, isipokuwa Joshua Mlundi aliyejisalimisha kanisani akiwa anaenda kutubu ndiyo vyombo vya dola vikajichukulia ujiko hapo.
Kila siku wanakomba kodi zetu na mafuta kumpeleka mahakamani, wanasema upelelezi haujakamilika na wamekataa Mulundi kunana na Ulimboka.
Hapa Ridhiwan amnong’oneze Mwenyekiti wa Chama kinachoongoza serikali kuwa utendaji huu sio sawa. Huu sio ushauri wangu, ni Watanzania tu wamenituma baada ya kusikia kauli yako Ridhiwan Kikwete.
Kwa mbali, umejaribu kuzungumzia na kutaka kuunganisha mauaji ya Morogoro na Iringa, na hiki kilichopo katika video ya Lwakatare. Sijui hayo kwa undani ila niseme ninayojua na ambayo Watanzania wote wanajua kuhusu mauaji ya Iringa.
Kuhusu mauaji ya Iringa, Tume ya Haki na Utawala Bora, inayolipwa kwa pesa za wapiga kura na walipa kodi, inayotambuliwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano iliyo chini ya Mwenyekiti wa CCM ambaye wewe Ridhiwani umaheshimu ilitoa kauli.
Jaji Ameir Manento alisema kuwa uchunguzi wa tume yake ambayo imepewa madaraka ya kusimamia utawala bora na haki za binadamu imebaini kuwa tukio la mauaji ya Mwangosi “limegubikwa na uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.”
Taarifa ya tume hiyo ilifafanua: “Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda tarehe 02/09/2012 katika utekelezaji wa majukumu yake alikiuka Sheria ya vyama vya siasa (Cap 258 RE. 2002) kifungu cha 11(a) na (b) na Sheria ya Polisi (Sura ya 322) kwa kuingilia kazi za OCD wa Mufindi na kutoa amri ya kuzuia shughuli za CHADEMA wakati yeye hakuwa “Officer In-charge” wa polisi wa eneo husika.
“Kwa maana hiyo amri aliyoitoa haikuwa halali kwa kuwa ilitolewa na mtu ambaye hakuwa na mamlaka kisheria kutoa amri hiyo. Haya ni matumizi mabaya ya mamlaka, hivyo ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.”
Jaji Manento aliongeza kwa msisitizo kwa kusema: “Kimsingi tume hii ya kudumu inamtaja Bw. Kamuhanda kama mhusika mkuu wa usababishaji wa mauaji ya Mwangosi na kuwa kutokana na uvunjaji wa wazi wa sheria vyombo vilivyo juu yake vinatakiwa kumchukulia hatua ikiwemo kuondolewa kazini na kufikishwa mahakamani kwa matumizi mabaya ya madaraka.
“Ni yeye aliyetoa amri ya kulipua mabomu ya machozi eneo lile, ambalo mojawapo ndilo linalodaiwa kumlipua Bw. Mwangosi.
“RPC aliamuru kupigwa kwa mabomu ya machozi ili kuwatawanya wananchi waliokusanyika katika ofisi za tawi hilo la CHADEMA.”
Haya ni maneno mazuri. Ulizia hapo hapo kwa mwenyekiti wa chama unayemheshimu kama vyombo vya dola vimechukua hatua kama unavyotaka. Hayo tu kwa leo nimeombwa nikuombe ufafanuzi kidogo kwa kuwa haujaeleweka.
chanzo:daima
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment