Wednesday, 14 November 2012

Katibu wa Mufti Zanzibar apelekwa India


KATIBU wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soroga amepelekwa nchini India kwa matibabu zaidi, huku hospitali alikopelekwa haijafahamika.
Sheikh Soroga alimwagiwa kemikali inayosadikiwa ni tindikali Novemba 6 mwaka huu saa 12:00 asubuhi nyumbani kwake Zanzibar akifanya mazoezi baada ya Swala ya Alfajiri.
Kabla ya kufikishwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), Sheikh Soraga alipatiwa matibabu kwanza Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Zanzibar.
Baada ya tukio hilo, viongozi wa ngazi mbalimbali wa serikali wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete walikwenda kumjulia hali, huku Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal akiwataka wananchi kuacha kuchukua sheria mkononi.
Ofisa Habari wa Moi, Jumaa Almas alisema Sheikh Soroga aliondoka Novemba 8, mwaka huu na kupelekwa India kwa matibabu zaidi.
“Siku ya Alhamisi Sheikh Soroga alitolewa hapa hospitalini,  huku wakidai wanampeleka India kwa matibabu zaidi,” alisema Almas.
Hata hivyo, Almas alisema hawajui hospitali alikopelekwa Sheikh Soroga na kwamba, iwapo watapata taarifa zaidi umma utajulishwa.
“India kuna hospitali nyingi kwakweli hatuna uhakika alikopelekwa, hivyo tukipata taarifa tutaweka wazi ili kila mtu ajue, ” alisema Almas.
Almas alisema uchunguzi wa kubaini aina ya kemikali aliyomwagiwa hadi sasa haijafahamika, ila kuwa uwezekano ikawa tindikali
chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment