Tuesday 25 December 2012

Albino azikwa dukani


CHAMA cha Watu wenye Ulemavu wa Ngozi Nchini (TAS), kimeitaka mahakama mkoani Mwanza, kutoa kibali cha kufukuliwa maiti ya mtoto mdogo, Witness Edward Omari (2), anayedaiwa kufariki kisha kuzikwa kinyemela saa sita usiku ndani ya duka wilayani Magu.
TAS imeitaka serikali mkoani hapa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, kuhakikisha inachukua hatua za makusudi ili mwili wa mtoto huyo albino anayedaiwa kufariki Desemba 15, mwaka huu, kwa ugonjwa wa malaria, sampuli zake zinapelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Mwanza, Ofisa Uhusiano wa TAS Taifa, Josephat Tona, alisema kuwa wameshtushwa na kitendo cha marehemu huyo kuondolewa katika Hospitali ya Wilaya ya Magu usiku na kuzikwa papo hapo.
Tona alisema hajawahi kuona mtu kafariki kisha kazikwa kwenye chumba cha biashara (dukani) na kwamba yeye na Mwenyekiti wa TAS Mkoa wa Mwanza, Alfred Kapole, walipata taarifa hizo kisha wakaenda hadi kwenye familia ya mtoto huyo na baadaye kuonyeshwa kaburi lake.
“Huyu mtoto albino alifariki kisha kuzikwa kwenye chumba cha kibiashara! Mbaya zaidi mwili wake ulichukuliwa saa 6 usiku mochwari kisha kwenda kuzikwa usiku huohuo bila majirani kushirikishwa.
“Baada ya kupata taarifa hizi, tuliwasiliana na Katibu wa TAS Magu, akatueleza yeye alikwenda kuhudhuria mazishi lakini baadaye akaambiwa tayari marehemu alishazikwa,” alisema.
Aliongeza kuwa baada ya kuambiwa hivyo, katibu huyo alipigwa butwaa na kuhoji marehemu amezikwa muda gani wakati yeye amekuwepo na hajaona akizikwa.
“Kutokana na utata huu wa mazishi ya mtoto albino, tumejawa hofu kubwa sana. Huenda kuna imani za kishirikiana zimetumika na pengine amekatwa baadhi ya viungo.
“Iweje achukuliwe hospitalini usiku na kuzikwa usiku huo huo tena bila watu kushirikishwa? Tunaitaka mahakama itoe idhini ya kufukuliwa mwili huo na upelekwe kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kufanyiwa uchunguzi zaidi,” alisisitiza.
Tona alifafanua kuwa zaidi ya albino wasiopungua 65 walishauawa kuanzia mwaka 2007 hadi sasa, huku makaburi 19 ya walemavu hao yakifukuliwa kwa imani za kishirikina, hivyo akaitaka serikali na vyombo vyake vya usalama, kuhakikisha vinadhibiti unyama huo.
Alisema kuwa tayari TAS ilishafungua jalada la uchunguzi katika kituo cha Polisi Magu na kituo cha polisi cha Kati jijini Mwanza kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria dhidi ya suala hilo.
Naye Mwenyekiti wa TAS Mkoa wa Mwanza, Alfred Kapole, Katibu, Mashaka Tuju, na mhasibu wa TAS mkoa, Anjelina Chuma, walieleza kusikitishwa sana na kitendo cha Witness kuzikwa kinyemela tena ndani ya duka.
Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi Makosa ya Jinai wa jeshi la polisi mkoani Mwanza (RCO), Joseph Konyo, alikiri kupokea malalamiko hayo kutoka kwa viongozi wa TAS, akisema kuwa amemwandikia barua mkuu wa upelelezi wa polisi wilayani Magu (OCCID), akimuagiza kufuatilia kwa karibu.
“Viongozi wa TAS wamekuja kwangu kunieleza, lakini nimemwagiza OCCID wangu wa Magu afuatilie suala hili kwa karibu sana. Nimemwagiza aende akajionee kaburi lilipo na apate maelezo ya kina...maana huyu mtoto hajauawa kwa makusudi bali amefariki kwa ugonjwa wa malaria, hivyo hii siyo kesi ya mada,” alisema.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment