Saturday 22 December 2012

Lulu ahamishiwa Mahakama Kuu


UPANDE wa serikali katika kesi ya kuua bila kukusudia inayomkabili msanii wa filamu nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’ jana ulimsomea kwa mapana kesi inayomkabili mshtakiwa huyo (Committal proceedings).
Wakili Mwandamizi wa Serikali, Shadrack Kimaro, mbele ya Hakimu Mkazi Augustina Mmbando, alimsomea Lulu maelezo ya mashahidi tisa na vielelezo ikiwemo ramani ya eneo la tukio kwenye chumba alichofia marehemu Kanumba, ripoti ya uchunguzi wa kifo na maelezo ya onyo ya Lulu.
Aliwataja mashahidi hao ni Sethi Kamugisha (24) ambaye alikuwa akiishi na Kanumba, Sophia Kassim (45) ambaye alimpangisha Kanumba, Dk. Paplas Kagaiga (29) ambaye alikuwa daktari wa Kanumba, Esther Zefania (40) askari polisi Oysterbay na Morris Sefwao mkazi wa Kijitonyama.
Wengine ni Mrakibu wa Polisi (ASP) Daniel Shilla kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kinondoni, Dk. Magreth Ibobo (40) ambaye aliombwa na familia ya Kanumba kusimamia upasuaji wa mwili, Inspekta Mwesiga (35) Afisa Uhamiaji kutoka kituo cha Horohoro, Tanga na Ditective Sajent Renatus wa kituo cha Polisi Oysterbay.
Akisoma maelezo ya onyo ya Lulu mbele ya Hakimu Mkazi Mmbando, wakili wa serikali, Shadrack Kimaro, alidai kuwa Lulu alitoa maelezo hayo Aprili 7 mwaka huu katika kituo cha polisi Oysterbay mbele ya askari wa kituo hicho, Ditektive Sajent Renatus.
Kimaro alidai Lulu alifahamiana na Kanumba kwa muda wa miaka 10 na walikuwa wakifanya kazi za sanaa ya uigizaji pamoja na Januari mwaka huu ndipo walipoanza rasmi mahusiano ya kimapenzi.
Wakili huyo alidai kuwa katika kipindi cha miezi minne ya mahusiano yao walikuwa wakigombana mara chache, lakini sababu kubwa ni wivu wa mapenzi kwa sababu wote walikuwa hawaaminiani katika mahusiano.
Pia wakili huyo alidai kuwa Aprili 5 mwaka huu Kanumba na Lulu walitumiana ujumbe mfupi wa simu wa kulaumiana.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment