Tuesday, 25 December 2012

Pikipiki zaua 771 kwa mwezi mmoja


WATU 771 wamekufa na wengine 4,562 kujeruhiwa katika ajali za pikipiki 4,637 zilizotokea kwa kipindi cha Novemba hadi Disemba mwaka huu.
Pia katika kipindi hicho mwaka 2010, jumla ya ajali za barabarani zilizoripotiwa zilikuwa 3,377 wakati mwaka 2011 ajali 3,326 zilitokea ambazo zilisababisha vifo vya watu 594 na kujeruhi 3034.
Takwimu hizo zilitolewa jana na Naibu Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Silima, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani alipokuwa akitoa tahadhari kwa madereva katika kipindi hiki cha kuelekea msimu wa sikukuu.
Aidha alisema kwa ajali za magari katika kipindi cha Novemba hadi Desemba mwaka 2010 zilizoripotiwa ni 3,377 na mwaka 2011 zikiwa 3,326 zilizosababisha vifo vya watu 594 na majeruhi 3034.
Kutokana na miezi hiyo kuwa mibaya zaidi, Naibu Waziri aliwataka madereva wa pikipiki na magari kuzingatia usalama zaidi wanapokuwa barabarani ili kuepusha athari zaidi za ajali.
Pia alitaja sababu mbalimbali zinazochangia ajali hizo kuwa ni pamoja na mwendo kasi, ulevi, uendeshaji wa hatari, ujazaji wa abiria na mizigo, kutofuata michoro na alama za barabarani na ubovu wa magari.

Kutokana na hali hiyo aliwataka madereva kuzingatia udereva wa kujihami, kuepuka mwendokasi, kuzingatia matumizi sahihi ya barabara kwa kuzingatia alama na michoro ya barabarani.
“Tumetoa takwimu hizi ili kuonyesha kuwa kuelekea msimu wa sikukuu kumekuwa na matukio mbalimbali ya ajali kutokana na madereva kutokuwa makini, kutozingatia alama za barabarani, ulevi na hata ushawishi unaotokana na abiria kufurahia mwendo kasi,” alisema Silima.
Alisema katika kipindi hiki cha kufunga mwaka watu wengi wanasafiri kuelekea mikoani hivyo kwa madereva waepuke kuendesha magari wakiwa wamechoka hasa wanaposafiri kwa kutumia magari madogo.
Alifafanua kuwa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Sumatra mikoani kote kwa sasa linaendelea na operesheni maalum inayolenga kudhibiti makosa mbalimbali yakiwemo ya upandaji wa nauli, kukiuka ratiba za safari, kutofunga mikanda ya usalama na makosa mengine.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment