Thursday, 7 February 2013

Dk. Cheni kumrejesha Lulu kwenye ‘game’ baada ya kutoka mahabusu



MSANII nyota wa filamu nchini, Mahfudh Hussein ‘Dk. Cheni’ amebainisha kuwa, hivi sasa wako katika maandalizi ya kucheza filamu na msanii Elizabeth Michael ‘Lulu’, aliyetoka mahabusu hivi karibuni.
Lulu alikuwa mahabusu tangu Aprili 7 mwaka jana, akikabiliwa na mashtaka ya kuua bila kukusudia, aliyekuwa msanii nguli, Steven Kanumba.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu juzi, Cheni alisema mpango huo umekuja baada ya Lulu kuwa nje ya ulingo wa filamu kwa zaidi ya miezi saba kutokana na kesi yake inayomkabili.
Alisema hivi sasa Lulu ana kiu ya kucheza filamu, ikiwa ni katika kudhihirisha kipaji chake, hivyo wamepanga atacheza na kulipwa kiwango cha juu cha fedha kama mchezaji nyota na siyo mchezaji aliyeshirikishwa.
“Tutamlipa fedha nyingi Lulu, kwa sababu yeye ni msanii nyota mwenye mvuto, huku jamii ikiwa na kiu ya kuona kazi zake ambazo hajazifanya kwa muda sasa,” alisema Cheni.
Alisema kuwa, katika filamu hiyo pia atakuwepo msanii Steve Mengele ‘Steve Nyerere’, ambaye kwa pamoja ndio waliojitokeza kumpa sapoti Lulu.
Katika hatua nyingine, Dk. Cheni ambaye yuko karibu zaidi na familia ya akina Lulu, alitanabaisha kuwa, tayari wameshampata mshauri nasaha kwa kumshauri Lulu ili aweze kurejea katika hali yake ya kawaida baada ya matatizo yaliyotokea.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment