Tuesday 26 February 2013

Katibu Mkuu Moravian avamiwa na majambazi Zanzibar

Watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi usiku wa kuamkia jana walivamia nyumba ya Katibu Mkuu wa Kanisa la Moravian Jimbo la Mashariki na Zanzibar Mchungaji Adolf Mwakanyamale eneo la chamazi jijini Dar es Salaam kwa lengo la kufanya uhalifu.

Akizungumza na Mwananchi Mwakanyamale alisema watu hao baada ya kufika katika eneo la tukio walianza kuvunja milango na ndipo alipoanza kupiga filimbi ya kuashiria hali ya hatari ili kuomba msaada kutoka kwa majirani,

Alisema majirani walipoanza kutoka ili kutoa msaada majambazi hayo yalifyatua risasi mbili hewani kwa lengo lakuwatisha hata hivyo majirani waliendelea kujitokeza kwa wingi eneo la tukio na ndipo majambazi hayo yakakimbia.

Wakati haya yakijiri taarifa za ndani katika kanisa hilo zimeeleza kuwa bodi ya dunia imefika jijini Dar es Salaam kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro unaoendelea kuchukua sura mpya ndani ya kanisa hilo.

Naye afande wa kituo cha Maturubai alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa walipokea taarifa ya tukio hilo na kisha kufika eneo hilo asubuhi ya jana na baada ya ukaguzi walifanikiwa kukuta maganda mawili ya risasi lakini hakuna mtu aliyejeruhiwa.

Alisema tayari wameshaandikisha kesi na kwamba kinachofanyika hivi sasa ni kuanza uchunguzi wa haraka ili kuweza kuwabaini watu waliohusika katika uvamizi huo.

wakati huohuo Mwenyekiti wa jimbo hilo Mchungaji Saul Kajura alisema Halmashauri yake imepata taarifa zisizorasmi za ujio wa uongozi wa umoja wa bodi ya dunia katika kanisa hilo.

"Tumesikia kuwa wanakuja, hatujui wanakuja kufanya nini, sisi tutawapokea lakini hatutahitaji kuzungumza nao kuhusu suala la mgogoro, kama wanahitaji kujua kuhusu mgogoro tutawaelekeza kwa jimbo mama, yaani jumbo la Kusini,"alisema Kajura.


Alisema kitendo cha bodi hiyo kuingia nchini kimya kimya bila kufanya mawasiliano yeyote na jimbo la misheni ni kinyume na taratibu  za kanisa hilo na kuonya kuwa badala ya kupunguza mgogoro kutaendelea kuchochea mgogoro ndani ya kanisa hilo.

Alisema hivi sasa wanasubiri kesi zilizopo mahakamani hivyo hawataweza kuzungumzia jambo lolote hadi kesi hizo zitakapo malizika.
chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment