Wednesday, 6 March 2013

POLISI WAMWEKA KATIKATI RAY C

Kamanda wa jeshi la polisi, kitengo cha kudhibiti madawa ya kulevya nchini, Godfrey Nzowa, amesema kuwa Ray C kila anapotembea anakuwa katikati ya askari wanaofuatilia nyendo zake.
“Kila anapokwenda, askari wamemzunguka. Tangu alipopata nafuu, tumekuwa tukihakikisha havutiwi na makundi mabaya, vilevile tunataka kuona kweli amejirekebisha,” alisema Nzowa na kuongeza:
“Ray C mwenyewe haoni lakini kila anapotoka, askari wanamuweka katikati. Kwa kifupi kipindi hiki tumemuweka katikati yetu, kwani hata anapokuwa nyumbani, tunachunguza nani anaingia na anapeleka nini.”
Nzowa aliongeza kuwa kitengo chake kimeamua kumuweka kati Ray C kwa sababu mbili, moja ikiwa kubaini na kuwanasa wauzaji wanaomharibu mwanamuziki huyo, pili ni kufuatilia kama msaada uliotolewa na Rais Jakaya Kikwete umefanya kazi yake ipasavyo.
“Mheshimiwa (JK) alitoa msaada wa matibabu kwa Ray C kwa nia njema, vilevile dada huyo aliapa mbele yake kama hatarudia tena. Sasa ni lazima kufuatilia na kudhibiti asije kuingia kwenye vishawishi, akakiuka kiapo na matokeo yake alichokifanya mheshimiwa kikaonekana hakina maana,” alisema Nzowa.
Kwa upande mwingine, Nzowa alisema, hali ya Ray C inaendelea kuimarika na akaongeza: “Akili yake imetulia, anaweza hata kutunga nyimbo tofauti na alivyokuwa. Watu ambao anafungamana nao kwa sasa ni wazuri, siyo magenge ya wauzaji na watumiaji wa madawa ya kulevya.”
Ray C, alisharipotiwa kuwa na hali mbaya baada ya kutopea kwenye utumiaji wa madawa ya kulevya.
Hata hivyo, JK aliamua kujitolea kunusuru maisha ya mwanamuziki huyo kwa kugharamia matibabu yake mpaka apone.
Takriban miezi mitatu iliyopita, Ray C alitinga ikulu na kumshukuru JK kwa msaada aliompa, vilevile akawaambia Watanzania kwamba sasa anajisikia amepona na anaweza kufanya kazi.
chanzo:.globalpublishers.info

No comments:

Post a Comment