Tuesday, 5 March 2013

Polisi wasaka wauaji wa kigogo UVCCM

Jeshi la Polisi mkoani Arusha linawasaka wanawake wawili kufuatia kifo cha kutatanisha cha mjumbe  wa Baraza Kuu  la Umoja wa Vijana wa  Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa kupitia Mkoa wa Arusha, Benson  Peter  Mollel (26).

Inadaiwa kuwa wanawake hao walikuwa na Mollel  kabla ya kufariki dunia ghafla juzi katika chumba cha hoteli moja jijini hapa.

Tukio hilo lilitokea mchana baada ya mwili wa merehemu kugunduliwa na wahudumu wa hotel hiyo walipotaka kukifanyia usafi chumba alichokuwa amelala marehemu huyo .

Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Arusha, Liberatus  Sabas, alisema jana kuwa marehemu alifika hoteli hapo, Machi 2 mwaka huu jioni na kupanga katika chumba namba 208.

Alisema Polisi baada ya kupata taarifa za tukio hilo, wanaendelea na msako kuwatafuta wanawake hao ambao walikuwa na marehemu kabla ya kukutwa na mauti ya ghafla.

Alisema kuwa mmoja wa wanawake hao alikwenda na marehemu hotelini hapo saa 7.00 usiku na mwingine alikwenda hotelini hapo asubuhi saa 5.00 asubuhi.

Sabas alisema polisi baada ya kufika hotelini hapo walimkuta marehemu na kuchukua mwili wake na kuhifadhi hospitali ya Mkoa Mount Meru.
chanzo:Nipashe

No comments:

Post a Comment