Friday, 19 April 2013

Bi. Kidude kama Tupac Shakur


MAISHA ya mwimbaji, Bi. Kidude, yamefikia ukomo Aprili 17, yakihusisha namba saba ambayo imewahi kufikisha ukomo wa msanii marehemu wa nchini Marekani wa kizazi cha sasa maarufu kama Tupac Omaru Shakur, aliyezaliwa Juni 16, 1971 na kufariki dunia Septemba 13, 1996.
Kifo cha mwanamama huyo kinafanana na Tupac kwa namba saba, kwa sababu matukio yaliyomtokea rapa huyo yalikuwa yakihusisha namba hiyo.
Kifo cha Tupac kilikuwa hivi; alipigwa risasi Septemba 7, miezi saba baada ya kuachia albamu yake ya ‘All Eyez On Me’, na alifariki dunia muda wa siku saba baada ya kupigwa risasi na alipigwa risasi saba na baada ya kifo chake ilitoka albamu yake iliyokuwa na jina la ‘The Don Killuminati’, ikimaanisha ‘Siku Saba za Nadharia’.
Hesabu ya miaka 25 ya 2pac aliyoishi kihesabu inahusishwa na namba saba (2+5=7) hata kifo chake kimahesabu kinaonesha alifariki dunia majira ya saa saba.
Namba hiyo inaonekana kwa Bi. Kidude kuanzia katika maisha yake binafsi ambapo alizaliwa Kijiji cha Mfagimarigo, Unguja katika familia ya watoto saba, amefariki dunia majira ya saa saba na maziko yake kufanyika majira ya saa saba. Pia aliolewa katika ndoa saba.
Maisha yake

Pamoja na umaarufu aliokuwa nao, lakini Bi. Kidude ameishi maisha magumu ambayo hayakwenda sambamba na hali yake halisi.
Maisha ya mkongwe huyo aliyeanza muziki mwaka 1920 yalikuwa ya kusikitisha kutokana na kutokuwa na hadhi ya jina lake linalotambulika ndani na nje ya nchi, kwani alikuwa akiishi katika nyumba ya hali ya chini iliyofikia hatua ya kumshinda kuimalizia huko eneo la Raha Leo, Zanzibar.
Hata katika moja ya mahojiano yake katika chombo kimoja cha habari cha hapa nchini, amewahi kusema kuwa pamoja na kuwa na sifa kubwa lakini maisha yake yamekuwa yakimhuzunisha kwa jinsi anavyoishi maisha duni.
“Mtu yeyote ayatazame maisha yangu aone anachoweza kunifanyia kwani niliweza kuitangaza Jamhuri (Tanzania) vema, kwa maana hakuna nchi ambayo sijawahi kuitembelea kwa ajili ya kueneza utamaduni wetu lakini bado maisha yangu hayafanani na kazi yangu,” alisema.
Kuzushiwa kifo
Amekuwa akizushiwa kifo mara kwa mara na mara ya kwanza kuzushiwa kifo ilikuwa Oktoba 26, 2011 ambapo ulisambazwa ujumbe kwenye mitandao ya simu za mkononi na mitandao ya kijamii, Facebook na Twitter kuwa Bi. Kidude amefariki dunia! Moja ya sms hizo ilisomeka kuwa: “Qaallu Inna Lillahi Wainna Ilaihi Raajiuni. BI. KIDUDE AMEFARIKI DUNIA!” Habari ambazo zilikanushwa na mwenyewe siku hiyo asubuhi.
Kifo chake
Akizungumzia kifo cha nguli huyo, Abdallah Baraka, ambaye ni mtoto wa kaka yake marehemu waliyeishi naye tangu akiwa mtoto jambo lililomfanya kumuita mama, alisema marehemu alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya kisukari kwa miaka mingi hadi mauti yanamkuta akiwa nyumbani kwake, Bububu mjini Zanzibar.
Baraka alisema siku kadhaa zilizopita hali yake haikuwa shwari na kuwalazimu kumpeleka hospitalini mara kwa mara kwa ajili ya kuangalia afya yake ambayo ilikuwa ikiwapa wasiwasi, mpaka juzi majira ya saa saba mchana mauti yalipomkuta.
“Mama yangu alikuwa anasumbuliwa na kisukari kwa muda mrefu ila siku za hivi karibuni hali yake haikuwa nzuri na kumkimbiza hospitalini mara kwa mara ili aweze kupona lakini imeshindikana kwani Mungu amempenda zaidi,” alisema Baraka.
Wasanii wanena
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wasanii wa muziki hapa nchini, Judith Wambura ‘Lady Jaydee’, Vicky Kamata na Linnah walisema hawaamini kama watapata mtu mwingine ambaye atakuwa mkongwe katika muziki kama alivyokuwa Bi. Kidude.
Lady Jaydee alisema hawezi kulisahau pengo la nguli huyo kutokana na kuishi naye vizuri katika tasnia ya muziki na kudai kuwa mpaka ilifikia wakati akaimba wimbo wake wa ‘Muhogo wa Jang’ombe’ ambao uliweza kumpa thamani zaidi katika tasnia ya muziki hapa nchini kutokana na maneno mazuri yaliyomo katika wimbo huo.
Anasema hataweza kumsahau kwa kuwa alimwahidi kumfundisha jinsi ya kutunga nyimbo ili aweze kuendeleza kipaji chake, zaidi ya hapo alipokuwa sasa, licha ya kuwa na uzoefu katika utunzi.
“Mimi kiukweli sitaweza kumsahau kwani alikuwa na mchango mkubwa kwa sisi chipukizi, mpaka kutupatia nafasi ya kuiga nyimbo zake, ni mtu ambaye alikuwa na moyo wa kipekee kabisa, ni pengo kubwa na tutazidi kumkumbuka,” anasema Jaydee na kuongeza kuwa kwa umri alioishi Bi. Kidude kwa kizazi cha sasa ni vigumu kufikisha umri huo.
Naye Linah anasema, wanadamu wanatakiwa kubadilika sasa, na kutambua uthamani wa mtu kabla mauti hayajamkuta na kuwataka Watanzania kumuenzi kwa kuthamini mchango wake katika taifa ikiwa ni pamoja na kuenzi nyimbo zake.
“Mtu kipaji chake kinatakiwa kutambuliwa mapema na si kusubiri mpaka afariki dunia ndipo sifa lukuki zinamiminika, cha muhimu tuwajali watu wakiwa hai na wao waweze kujithamini kutokana na mchango ambao wanautoa hapa nchini,” anasema Linnah.
Mbali na wasanii hao, Vicky Kamata ambaye ni msanii na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), anasema kifo cha Bi. Kidude ni pengo kubwa kwa taifa na wasanii kwa ujumla kutokana na mchango wake, hasa kuwapa sapoti kubwa vijana ambao bado wanachipukia katika fani hiyo.
“Huyu bibi alikuwa hana ubaguzi kabisa, kwani hata majukwaani alikuwa akijipanga na watoto na kufanya nao shoo bila ya kuwa na upendeleo wowote, kiukweli mfano huo ni wa kuigwa na waliobaki,” anasema Kamata.
Huku Nasseb Abdul ‘Diamond’ jana aliungana na maelfu ya watu waliofurika katika mazishi ya kikogwe huyo aliyekuwa na zaidi ya miaka 90 aliyefariki dunia kwa ugonjwa wa kisukari ambao umemsumbua kwa muda mrefu katika makaburi ya Kitumba mjini Zanzibar.
Diamond aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii (Facebook) kuwa amejitahidi kadiri awezavyo hadi kuhudhuria mazishi ya nguli huyo kwa madai kuwa jambo hilo linaweza kumkuta mtu yeyote.
Historia yake
Bi. Kidude alikuwa gwiji wa muziki katika Bara la Afrika, na kujulikana kwa rika zote kutokana na umaarufu wake wa kutumbuiza jukwaani, mkongwe huyo katika fani ya muziki huo wa mwambao.
Muziki huo umechanganywa na vionjo kutoka Uarabuni na Afrika na umejikita katika mwambao wa Afrika Mashariki, yaani Zanzibar, Mombasa, Lamu na kwingineko huku Bara ukijikongoja.
Fatuma binti Baraka au Bi. Kidude, amezaliwa katika Kijiji cha Mfagimarigo Zanzibar katika familia ya watoto saba, baba yake mzee Baraka alikuwa mfanyabiashara wa nazi, zao ambalo linategemewa sana mjini Zanzibar.
Kuhusu tarehe rasmi ya kuzaliwa kwake Bi. Kidude aliwahi kusimulia kuwa hafahamu tarehe halisi aliyozaliwa, isipokuwa anachojua ni kwamba alizaliwa wakati rupia ikitumika kama fedha. Wataalamu wa mahesabu baada ya kupata taarifa hizo wakampigia mahesabu na kumkabidhi miaka yake kwamba ni zaidi ya miaka 90.
Katika historia yake enzi za uhai wake, Bi. Kidude alisema uimbaji aliuanza tangu alipokuwa na umri wa miaka kumi na alijifunza kutoka kwa msanii mkongwe na aliyetamba sana enzi hizo, Sitti binti Saad.
Anasema wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali walikuwa wakifika Zanzibar kuja kumwona Sitti, na kwa vile Bi. Kidude na Sitti walikuwa wako karibu, basi yeye alikuwa akiwapeleka wageni wale nyumbani kwa Bi. Sitti, wakifika huko wageni walikuwa wakiingia ndani na yeye kubakia nje.
Huko ndani Bi. Sitti alikuwa akiwaimbia wale wageni, na yeye akiwa nje akimsikiliza kwa makini, akimfuatisha jinsi alivyokuwa akiimba na kutumia nafasi hiyo ambayo ilimfanya kupata umaarufu zaidi. Aliendelea hivyo hadi akawa mahiri sana katika uimbaji.
Alipokuwa na miaka 13, kwa mara ya kwanza alitoroka nyumbani kwao Zanzibar na kukimbilia Tanzania Bara, baada ya kulazimishwa kuolewa.
Lakini alipokuwa kigoli wa kutosha kuolewa aliolewa ingawa ndoa hiyo nayo haikudumu kutokana na manyanyaso aliyokuwa akiyapata, hivyo aliamua kukimbilia kaskazini mwa Misri ikiwa ni katika miaka ya 1930, huko aling’ara sana katika fani yake ya uimbaji na uchezaji ngoma.
Lakini ilipofika miaka ya 1940 aliamua kurudi nyumbani Zanzibar ambako aliendelea na shughuli zake za uimbaji.
Bi. Kidude alikuwa hategemei kazi moja pekee ya uimbaji, kwani pia alikuwa mfanyabiashara ya ‘wanja’ na ‘hina’ ambavyo alivitengeneza yeye mwenyewe, pia alikuwa mtaalamu wa matibabu ya dawa za miti shamba na zaidi ya hayo alikuwa mwalimu mzuri sana wa unyago na alianzisha chuo chake mwenyewe na anasema katika wanafunzi wake wote hakuna aliyepata talaka kutoka kwa mumewe.
Vileo
Pamoja na umri wake mkubwa, lakini Bi. Kidude alikuwa mbishi kuacha tabia yake ya kuvuta sigara na kunywa pombe, jambo ambalo ni nadra kukutwa likifanywa na wanawake wa Zanzibar.
Mara kadhaa alikuwa akipinga kuacha akieleza kwamba vilevi hivyo amekuwa akivitumia kwa muda mrefu lakini hakuwahi kuona madhara yake.
Bi. Kidude amefanikiwa kufanya maonesho katika nchi nyingi ikiwamo Oman, Ufaransa, Hispania, Ujerumani na Uingereza.
Tuzo
Amekwisha pata tuzo mbalimbali ikiwamo ya Tamasha la Filamu la Nchi za Jahazi (ZIFF), mwaka 1999 ikiwa ni tuzo ya maisha. Tuzo nyingine kubwa ya kimataifa aliyotunukiwa mwaka 2005 ni iliyojulikana kama WOMAX, iliyotambua mchango wake katika muziki na utamaduni wa Zanzibar.
Mwimbaji huyo alipewa nishani ya sanaa ya heshima na Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete, mwaka jana akitambua mchango alioutoa kwa ajili ya maendeleo ya taifa na kimataifa.
Nyimbo
Nyimbo alizowahi kuimba ni pamoja na ‘Muhogo wa Jang’ombe’ alioimba kwa Kiswahili na Kiarabu, ‘Yalaiti’, ‘Kijiti’, ‘Beru’ na nyingine nyingi alizoshirikishwa kama ‘Ahmada’ wa ‘Offside Trick’.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment